De Reuck, Kante ‘wampotezea’ Fadlu kiaina

NYOTA wapya wa Simba, kitasa Rushine De Reuck na Allasane Kante wamewatuliza mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kuondoka kwa Kocha Fadlu Davids wakisema kila kitu kitakaa sawa kwa vile wachezaji wamejipanga kuendeleza moto wa Msimbazi katika mechi za ndani na za kimataifa.

De Reuck aliyefunga bao la kwanza la Simba katika mechi ya juzi usiku ya Ligi Kuu dhidi ya Fountain Gate alisajiliwa na Fadlu dirisha lililopita akitokea Mamelodi Sundowns ya Sauzi alisema mabadiliko ya benchi la ufundi ni sehemu ya soka na jukumu la wachezaji ni kuipigania timu.

“Mimi nipo hapa kwa ajili ya Simba. Kocha anaweza kubadilika lakini timu inabaki ile ile. Kazi yangu ni kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha tunapata matokeo,” alisema De Reuck aliyeanza kuonyesha ubora tangu mechi ya Simba Day dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, kisha kuonyesha kiwango kikubwa Ngao ya Jamii, licha ya Simba kupoteza kwa bao 1-0 kwa Yanga.

Beki huyo wa kati alisema mashabiki wa Simba wanapaswa kuwa na imani kwa sababu kikosi kilichopo kina ubora na uzoefu wa kucheza mashindano makubwa.

“Hii ni Simba, ni timu kubwa na kwa bahati nzuri nilikuwa nikiona kile inafanya katika mashindano ya kimataifa. Tunapaswa kutulia na kuendelea kushirikiana, naamini tutafanikisha malengo yetu msimu huu,” alisema De Reuck, huku kiungo mkabaji, Alassane Kanté anayepambana kuingia kikosi cha kwanza cha timu hiyo alikazia kwa kusema; “Soka ni safari ndefu. Tunachopaswa kufanya ni kujikita katika mechi zetu. Kocha mpya akija tutamuheshimu na kumsaidia, lakini kwa sasa akili zetu zote zipo kwa mchezo wa Jumapili,” alisema Kanté.

Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Botswana, Simba iliibuka na ushindi wa bao 1-0 kupitia goli la Ellie Mpanzu, mechi hiyo pia ilikuwa ya mwisho kwa Fadlu kukaa benchi la wekundu hao kabla ya kuhamia Raja Casablanca ya Morocco.

Kanté alisema mechi ya marudiano itakuwa tofauti kwani wanatarajia kupewa sapoti kubwa ya mashabiki wao wa nyumbani.

“Tunajua mashabiki watatupa nguvu ya ziada. Tunahitaji kutumia nafasi zetu mapema ili kuondoa presha,” alisema.

Kwa sasa Simba ipo chini ya kocha wa mpito, Hemed Suleiman ‘Morocco’ akisaidiwa na Seleman Matola.

Akiongelea mchakato wa kocha mpya wa Simba, Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Zubeda Sakuru alisema upo pazuri na siku chache zijazo watatoa taarifa rasmi, akiwataka Wanasimba kuwa watulivu.

“Mashabiki wetu wanatakiwa kujua viongozi tunafanya kile ambacho kinawezekana, ili kuendelea na mapambano ya msimu huu kwa kiwango kile kile tulichojiwekea, hakuna ambacho kitaharibika,” alisema Zubeda.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni Simba inatarajia kukamilisha uteuzi wa kocha mpya wiki ijayo kuchukua nafasi ya Fadlu aliyeondoka Msimbazi akiwa ameifikisha timu hiyo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza kwa mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco iliyobeba taji.