Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Ruwa’ichi amewataka Watanzania kutozoea kifo kwani watakuwa viumbe wa ajabu.
Askofu Ruwa’ichi ametahadharisha endapo watu watajenga mazoea dhidi ya kifo, watasababisha mauaji ya binadamu wenzao kwa mzaha.
Kiongozi huyo ametoa wito huo leo Jumamosi Septemba 27, 2025 wakati wa misa maalumu ya kumuaga hayati Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa, Mtanzania aliyewahi kuhudumu kama Balozi wa Papa katika nchi mbalimbali duniani.
Askofu Rugambwa aliyefariki dunia wakati akipatiwa matibabu huko Roma, Italia usiku wa Septemba 16, 2025, mwili wake umewasili nchini jana Septemba 26, 2025 kutoka nchini Italia.
“Tunapoadhimisha msiba huu tusiwe na uzuni iliyopitiliza imani yetu itufariji na kutuongoza kama walivyo mitume na sisi tuna mahangaiko yetu, lakini kamwe tusizoee kifo tulizoea kifo tutakuwa viumbe wa ajabu, ukizoea kifo utakuwa na uwezekano wa kumuua mwenzako kimzahamzaha kama mbuzi,” amesema.

Askofu Ruwa’ichi amesema uhai wa binadamu una thamani kubwa machoni kwa Mungu, akisisitiza kifo kibaki kuwa fumbo machoni mwa binadamu na kamwe isiwe mazoea.
Akimueleza Askofu Rugambwa, Askofu Ruwa’ichi amesema alikuwa askofu ndani ya kanisa, masuala ya diplomasia na atakumbukwa kwa kazi yake ya uinjilishaji na kuhimiza mshikamano baina ya watu kwenye jamii.

“Ni Mtanzania wa kwanza kuingizwa kwenye orodha ya wawakilishi wa Baba Mtakatifu, Balozi wa Vatican duniani kupitia yeye tumepewa fursa kama Kanisa la Tanzania, tunamshukuru kwa utumishi wake huu, tumuombee kwa Mungu amsamehe mapungufu yake,” amesema.
Baada ya Misa ya kuagwa kwa askofu huyo, misa ya mazishi itafanyika Kanisa Kuu Katoliki Jimboni Bukoba, Jumatatu Septemba 29, saa 3:30 asubuhi.
Huyu hapa Askofu Rugambwa
Askofu Mkuu, Rugambwa ambaye amefariki dunia usiku wa Septemba 16, 2025 wakati akipatiwa matibu Roma nchini Italia, ni Mtanzania mzaliwa wa Mkoa wa Kagera.

Azaliwa Oktoba 8, 1957 mkoani Kagera na kuwekwa wakfu katika daraja takatifu ya upadri Julai 6, 1986 na Askofu Nestorius Timanywa wa Jimbo Katoliki Bukoba (kwa wakati huo).
Baada ya masomo ya dini, alipewa daraja takatifu ya upadri mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986.
Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican Julai Mosi, 1991.
Juni 28, 2007 Papa Benedikto wa XVI alimteua kuwa Katibu Mkuu Msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalumu.

Februari 6, 2010, Papa Benedikto XVI, alimteua tena kuwa Askofu Mkuu na Balozi wa Vatican nchini Angola, Sao Tome na Principe na kuwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu Mkuu wa Vatican kwa wakati huo, Machi 18, 2010.
Machi 5, 2015 akateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Honduras na Machi 29, 2019, Papa Francisko akamteua kuwa Balozi wa Vatican nchini New Zealand na mwakilishi wa kitume kwenye visiwa vya Bahari ya Pacific.
Machi 30, 2021, Papa Francisko alimwongezea majukumu kwa kumteua kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Jamhuri ya Microsia, iliyoko Magharibi mwa Bahari ya Pacific.
Wakati huohuo aliendelea kuwa Balozi wa Vatican kwenye Visiwa vya Marshall, Kiribati, Nauru na Tonga.
Pia, nafasi nyingine aliyowahi kuhudumu ni Balozi wa Vatican nchini New Zealand, Fiji, Palau na hatimaye Mwakilishi wa Kitume kwenye Bahari ya Pacific.