Jaji amkumbusha DPP kukagua mahabusu za Polisi

Geita. Jaji Griffin Mwakapeje wa Mahakama Kuu, Kanda ya Geita, amemkumbusha Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mahabusu za Polisi ili kubaini wanaoshikiliwa kinyume cha sheria.

Hatua hiyo ni baada ya jaji kubaini mtoto wa marehemu kushikiliwa mahabusu ya Polisi kwa siku 62 bila kuelezwa kosa lake, licha ya kuwa mshukiwa mkuu wa mauaji ya mama yake ambaye ni baba yake mzazi alikuwa ametiwa mbaroni na polisi.

Jaji Mwakapeje ametoa kauli hiyo Septemba 25, 2025 katika hukumu ya kesi ya mauaji ya Kabula Mathias, iliyokuwa ikimkabili Daud Gwanchele na Wilson Madoshi, ambao wameachiwa huru kwa kukosekana ushahidi dhidi yao.

Akitoa ushahidi wa kumtetea Gwanchele ambaye ni baba yake mzazi, shahidi wa pili wa utetezi, Msemakweli Gwanchele alisema yeye ndiye aligundua mwili wa mama yake, ukiwa umelala kifudifudi Agosti 11, 2024.

Baada ya kuona mwili huo ukiwa umenyongwa kwa kanga, alimpigia simu baba yake kumjulisha na baadaye polisi walimhoji na kumweka mahabusu kuanzia Agosti 11, 2024 hadi Oktoba 12, bila kumweleza ni kwa nini anashikiliwa. Msemakweli hakuwa sehemu ya washtakiwa wa kesi hiyo ya mauaji.

Akihitimisha hukumu iliyomwachia huru baba yake na mshitakiwa mwenzake, jaji amemkumbusha DPP wajibu wake wa kisheria wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mahabusu za Polisi ili kuhakikisha haki zao zinapatikana.

Wajibu huo wa DPP kwa mujibu wa Jaji Mwakapeje, unapatikana katika kifungu cha 17(4) cha Sheria ya Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS) sura ya 430 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023. DPP ana ofisi mikoa yote kupitia NPS.

Ukaguzi huo kwa mujibu wa jaji utasaidia kulinda haki za washukiwa waliopo mahabusu, ikiwa ni wajibu wake wa kusimamia haki jinai.

“Upungufu wa namna hii, hasa katika kesi zinazohusu watoto wadogo au vijana wanaozuiliwa bila uhalali, lazima ushughulikiwe haraka ili kuzuia kujirudia na kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki za kimsingi na utawala wa sheria,” amesema.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulidai mshtakiwa wa kwanza (Daud) alimshuku mkewe kwa uzinzi na uchawi, hivyo akamkodi mshitakiwa wa pili (Madoshi) kwa Sh200,000 ili amuue mkewe.

Jaji Griffin Mwakapeje wa Mahakama Kuu, Kanda ya Geita



Ilidaiwa mshtakiwa wa kwanza alilipa malipo ya awali ya Sh30,000, madai ambayo yalikanushwa na washtakiwa, hivyo kuulazimu upande wa mashtaka kuita mashahidi wanane kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Shahidi wa kwanza, Dunia Buzinza, mwenyekiti wa Kijiji cha Chigunga, alieleza Agosti 11, 2024 saa 1:45 asubuhi alipigiwa simu akajulishwa kuhusu kuokotwa mwili wa mtu kwenye shamba la mshtakiwa wa kwanza.

Alipofika eneo la tukio alikuta wanakijiji wamekusanyika na waliutambua mwili kuwa wa Kabula Mathias, ukiwa na michubuko shingoni, damu zikimtoka puani na akiwa amefungwa kwa kitenge shingoni.

Shahidi wa pili, Mapinduzi Kasigwa, mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyakaswa, alieleza Julai 2024, Kabula (marehemu) alimfuata akamweleza kwa siri kuwa mumewe anamshuku kwa uzinzi na uchawi.

Alimwambia iwapo atauawa, basi atakayehusika na kifo chake ni mumewe, hivyo Agosti 11, 2024 alipojulishwa kuhusu kifo cha mwanamke huyo aliwajulisha polisi waliofika eneo la tukio.

Mashahidi wengine walieleza namna walivyopata taarifa za kupatikana kwa mwili wa Kabula na majeraha aliyokuwa nayo, huku wale wa kutoka Jeshi la Polisi walieleza namna walivyopeleleza tukio hilo na kuwakamata washtakiwa.

Shahidi wa kwanza wa utetezi, Simon Daud, ambaye ni mtoto wa mshtakiwa wa kwanza, alieleza Agosti 9, 2024 alisafiri na baba yake kwenda Sengerema na walikaa huko hadi Agosti 11, 2024 walipopokea taarifa za msiba wa mama yake.

Walirudi nyumbani siku hiyohiyo saa 11:00 jioni, baadaye polisi walifika na kumkamata baba yake akiwa katika maziko ya mama yake, huku shahidi wa pili, Msemakweli akieleza alivyougundua mwili wa mama yake kisha naye kukamatwa.

Shahidi wa tatu wa utetezi alikuwa mshtakiwa, Daud Gwanchele ambaye alisema wakati mauaji yanatokea alikuwa Sengerema na alirudi Agosti 11 na kujikuta akitiwa mbaroni na polisi wakiwa katika shughuli ya mazishi.

Alieleza polisi walimtesa na kumpiga, huku wakimning’iniza kichwa chini miguu juu. Alikana kumuua mkewe wala kuwasiliana na Madoshi, akisisitiza maelezo aliyoandika polisi, aliyaandika baada ya kuteswa.

Mshitakiwa wa pili alijitetea akieleza Agosti 15, 2024 akiwa anarudi nyumbani alivamiwa na watu asiowajua ambao walichukua simu na fedha, baadaye alipelekwa Kituo cha Polisi Katoro alikomkuta mshtakiwa wa kwanza.

Alidai Polisi walimtuhumu kwamba alilipwa fedha ili kumuua Kabula, tuhuma alizozikana. Vilevile, alidai alipigwa na kulazimishwa kuweka dole gumba katika maelezo yaliyoandikwa na Polisi pasipo kupewa fursa ya kuyasoma.

Alidai aliendelea kushikiliwa polisi hadi Oktoba 2, 2024 alipofikishwa mahakamani akashtakiwa kwa mauaji ya Kabula, shtaka alilolikana pamoja na kulipwa ili kutekeleza mauaji hayo.

Jaji amesema ni wajibu wa upande wa Jamhuri kuthibitisha hatia ya washtakiwa pasipo kuacha shaka, lakini katika kesi hiyo, ulishindiwa kuthibitisha vigezo muhimu vinavyotengeneza kosa la mauaji ya kukusudia.

Jaji amesema kwa kuzingatia ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri, kifo cha Kabula kinathibitishwa pasipo shaka kutokana na ushahidi wa mashahidi licha ya kwamba ripoti ya uchunguzi wa kifo chake haikupokewa kama kielelezo.

Kuhusu iwapo washtakiwa wanahusika na mauaji hayo, amesema ushahidi umeshindwa kuwaunganisha, kwani hakuna shahidi awe ni ndugu, jirani au maofisa wa Polisi waliotoa ushahidi waliwaona washtakiwa wakimuua Kabula.

Akichambua ushahidi huo, amesema shahidi wa pili wa mashtaka ambaye alidai kuwa na taarifa ya vitisho dhidi ya Kabula (marehemu), hakuripoti taarifa hiyo kwa mamlaka wala hata kumwambia jirani au ndugu yeyote wa karibu wa familia.

Katika kesi hiyo, jaji anasema hakuna jirani yeyote aliyetoa ushahidi akisema aliwahi kushuhudia au kusikia uwepo wa mgogoro wowote kati ya mshtakiwa wa kwanza na Kabula jambo linalothibitisha hapakuwapo kutokuelewana.

Shahidi wa pili wa utetezi ambaye ni mtoto wa kwanza wa marehemu alieleza hakujawahi kuwapo kutoelewana kati ya baba na mama yake au familia hiyo.

Kuhusu maelezo ya mshtakiwa wa kwanza aliyoyaandika polisi kuwa alikiri kuhusika na mauaji hayo na kumtaja pia mshtakiwa wa pili, jaji amesema maelezo ya ushahidi huo yalipaswa kuungwa mkono na ushahidi huru.

Vilevile, amesema hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa ama Daud Gwanchele au Wilson Madoshi, walifanya tendo la mauaji, hivyo Jamhuri imeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao. Amehitimisha kwa kuwaachia huru washtakiwa.