Unguja. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema kutokana na changamoto ya mmomonyoko wa maadili inayowaathiri vijana wa vyuo vikuu, wanapaswa kupewa uelewa wa namna ya kukabiliana na janga hilo.
Amesema hayo leo Jumamosi Septemba 27, 2025 akifunga mkutano wa 43 wa Chama cha Washauri Wanafunzi Tanzania (Taccoga1984), uliofanyika Maruhubi, mjini Unguja.
Profesa Mushi amesema chama hicho ndicho chenye dhamana ya kufanya hivyo, kwani kimebeba mambo matatu yakiwamo afya ya akili kwa wanafunzi, maadili na mtazamo chanya wa vijana.
Amesema bila ya vijana kuwa na maadili, hakiwezi kupatikana kizazi chenye mustakabali mzuri wa elimu na viongozi bora.

Mwenyekiti wa Chama Cha washauri wanafunzi Tanzania (Taccoga1984), Sophia Nchimbi akizungumza wakati wa ufungaji wa mkutano wa 43 wa chama hicho. Picha na Zuleikha Fatawi
“Vijana wengi wanadhani maisha wanayoishi wasanii ni rahisi ndiyo sababu inayowafanya kuishi nje ya maadili, hivyo naomba msukumo mkubwa uwekwe katika hilo ili wasiendelee kuharibiwa na utandawazi,” amesema.
Profesa Mushi amesema wizara inatambua Taccoga1984 ni chombo cha usalama, nidhamu, huruma na utulivu, si kwa wanafunzi pekee bali hata kwa taasisi kwa ujumla, hivyo wanapaswa kuhakikisha wanafunzi wote, wakiwamo wenye mahitaji maalumu wanapata msaada stahiki.
Amekisihi chama hicho kutumia maarifa, ubunifu na mbinu mpya za kidijitali ili kuwahudumia wanafunzi kwa ufanisi zaidi.
Vilevile, amesema huduma zinazotolewa zinaendana na dira ya taifa ya kujenga rasilimali watu yenye maadili na uzalendo, kwa hiyo washauri na maofisa wana jukumu la kuhakikisha vijana wanalelewa kimaadili na kisaikolojia sambamba na taaluma zao.
Amesema wizara ipo tayari kushirikiana nao kwa kuzidisha jitihada za kuwaendeleza kupitia mafunzo na kujengea uwezo, hususani katika maeneo ya malezi ya makundi maalumu na uboreshaji wa huduma za wanafunzi.

Wanachama wa chama cha washauri wanafunzi Tanzania waliohudhuria mkutano wa 43 wa chama hicho. Picha na Zuleikha Fatawi
Mlezi Msaidizi wa Taccoga1984, Rehema Horera amesema chama hicho kina jukumu kubwa la kulea wanafunzi kwa kuwafanya watulie na kuendelea na masomo yao vizuri.
Mshiriki wa mkutano huo, Zitta Victoria Mnyanyi, amesema mmomonyoko wa maadili ni miongoni mwa janga linalohitaji kushughulikiwa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Amesema, chama hicho kimekuwa jukwaa muhimu la kuunganisha nguvu za pamoja katika kupambana na changamoto mbalimbali na kusaka mbinu za kuyatatua matatizo yanayowakabili wanafunzi.
Mwenyekiti wa Taccoga1984, Sophia Nchimbi amesema chama hicho chenye wanachama 63 kimekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake, ikiwamo kuendesha mikutano, kutoa mafunzo na kupata ofisi katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Ametoa wito kwa vyuo kushiriki na kujiunga na chama hicho kwa lengo la kujiimarisha kwa kusaidiana kutatua changamoto zinazojitokeza kwa wanafunzi wa vyuo.
Utafiti uliozinduliwa Januari 26, 2023 na Taasisi ya Regional Education Learning Initiative (Reli) kwa kushirikiana na Taasisi ya Uwezo Tanzania ulionyesha kundi kubwa la vijana nchini halina maadili na stadi za maisha.
Ripoti hiyo yenye jina: “Mchanganuo wa stadi za maisha na maadili katika Afrika Mashariki” uliofanyika Julai, 2022 ilihusisha vijana kuanzia umri wa miaka 13 hadi 17 katika wilaya 34, kaya 11,802 zikihusika na vijana 14,645 walihusishwa kutoka Tanzania Bara.
Utafiti huo ulionyesha kijana mmoja pekee kati ya 10 ana heshima na kujali maadili katika jamii, ambayo ni sawa na asilimia 12.5 ya vijana wote waliohusika katika utafiti huo.
Vilevile, utafiti huo ulionyesha kuwapo uelewa mdogo wa vijana kujitambua na kutatua tatizo, asilimia 16.8 pekee wakiwa ndio wenye uwezo huo.