Mgombea urais CUF awaonya wanaohamasisha maandamano Oktoba 29

Tanga. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Gombo, amewatahadharisha wale wanaohamasisha maandamano siku ya kupiga kura, Oktoba 29, 2025, akisema nia yao ni kuichafua Tanzania huku wao wakiwa salama nchi za nje.

Gombo ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi Septemba 27, 2025, wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika mkoani Tanga, alipokuwa akitoa tathmini ya awamu ya kwanza ya kampeni zake alizozifanya katika mikoa 14 ya Tanzania Bara na Visiwani.

“Wanaohamasisha maandamano hawako Tanzania. Wanataka kuona vurugu, wakati wao wako salama kwenye kumbi za starehe nje ya nchi. Watanzania wasikubali kutumika,” amesema Gombo.

Mgombea huyo wa CUF amewasihi Watanzania wote kupuuza miito ya maandamano, badala yake wajitokeze kwa wingi katika vituo vya kupiga kura ili kufanya maamuzi ya kidemokrasia kwa njia ya amani.

“Njia pekee ya kuiondoa CCM ni kupitia sanduku la kura, siyo kwa maandamano wala kususia uchaguzi. Watanzania wajitokeze kumpigia kura diwani, mbunge na rais kupitia CUF kwa ajili ya mabadiliko ya kweli,” amesisitiza.

Gombo pia ametoa wito kwa vijana kutokubali kushawishiwa na propaganda za mitandaoni zinazolenga kuvuruga uchaguzi, akieleza kuwa demokrasia ya kweli hujengwa kwa ushiriki, si kwa vurugu.

“Wanahamasisha maandamano siku ya kupiga kura, wanaohamasisha wapo nje ya nchi, wananchi wasikubali nchi iingie katika vurugu na machafuko…njia pekee ni kujitokeza kupiga kura za kunichagua kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, madiwani pamoja na wabunge wengi wa CUF Ili niweze kuunda Serikali yenye kujali matatizo ya wananchi,” amesema Gombo.

Amesema kama akichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania atahakikisha anatoa ajira kwa vijana, matibabu yatakuwa bila malipo na elimu kuanzia  chekechea hadi chuo kikuu itatolewa bure Kwa wanafunzi wote.

“Tanzania si maskini kama inavyoonekana, ina raslimali za kutosha, kama nitapata ridhaa ya kuunda  Serikali kupitia CUF nitahakikisha Watanzania wanatibiwa bila malipo, elimu kuanzia chekechea hadi chuo kikuu itatolewa bure na nitahakikisha ajira inatolewa kwa vijana bila kupendelea watoto wa wakubwa kama inavyofanyika hivi sasa,” amesema Gombo.

Mgombea huyo wa urais kupitia CUF amesema iwapo atachaguliwa kushika nafasi anayoiwania atahakikisha mara atakapoapishwa anasimamia uundwaji wa katiba mpya itakayokidhi matakwa ya sasa.

“Sitasubiri siku mbili au 100, nikiapishwa tu nitahakikisha mchakato wa uundwaji wa katiba mpya unaanza kwa kuwa ndiyo kilio kikuu cha watanzania Kwa sasa,” amesema Gombo.