Polisi Kigoma kuchunguza wanaokusanya vitambulisho vya mpigakura

Kigoma. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma limeanzisha uchunguzi kuhusu tuhuma za ukusanyaji haramu wa vitambulisho vya mpiga kura katika Jimbo la Kigoma Kaskazini.

Tuhuma hizo zinamhusisha baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wanaodaiwa kupita mitaani, wakilaghai wananchi kukusanya na kuandikisha namba za vitambulisho vyao vya kupiga kura.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Filemon Makungu, katika taarifa yake ya leo Septemba 27,2025 kupitia mitandao rasmi ya jeshi hilo amethibitisha kuwa matukio haya yametokea katika kata mbalimbali ikiwemo Mwandiga, Kagunga, Simbo, Mkigo, Kagongo na Kidawe.

Taarifa hiyo imefafanua kuwa vitendo hivyo ni kosa la kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2024, chini ya kifungu cha 14 (1) (g) na 119 (2) cha Sheria Na. 1 ya mwaka 2024.

Kamanda Makungu amesema uchunguzi wa tuhuma hizo unaendelea na pindi utakapokamilika na kubaini ukweli wa tuhuma hizo,  wote watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kwa mujibu wa Makungu, Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuwa watulivu na kushirikiana na vyombo vya dola ili kuhakikisha uchunguzi unafanyika kwa ufanisi na wahusika wanashughulikiwa ipasavyo.

Siku za nyuma kumekuwa na madai ukusanyaji wa vitambulisho vya mpigakura kwa watu mitaani hali iliyojenga hofu kwamba kitendo hicho ni uvunjaji wa sheria.

Baadhi ya watu walijenga hofu kuwa kuandika namba za vitambulisho kunaweza kukawa na nia ya kuwadanganya wapigakura, huku wengine wakihusisha kwamba taarifa hizi zinaweza kutumiwa vibaya.