Arusha. Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, imemuachia huru raia wa Nigeria, Onyebuchi Ernest Ogbu, aliyekuwa akikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 15.79.
Onyebuchi na mwenzake, Henry Ogwunyi (ambaye alifariki dunia akiwa mahabusu), wote wakiwa raia wa Nigeria, walifikishwa mahakamani kwa shtaka hilo. Baada ya kifo cha mwenzake, kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 5757/2024 iliendelea dhidi ya Onyebuchi pekee.
Hukumu ya kesi hiyo ilisomwa Septemba 26, 2025 na Jaji Monica Otaru, huku nakala ya hukumu hiyo ikichapishwa kwenye mtandao wa mahakama siku hiyohiyo.
Katika uamuzi wake, Jaji Otaru alisema baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa, Mahakama imebaini kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha shtaka dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote.
“Mahakama haijaridhishwa na ushahidi uliotolewa, hivyo mshtakiwa anaachiwa huru,” alisema Jaji Otaru.
Aidha, Mahakama iliamuru mshtakiwa akabidhiwe hati yake ya kusafiria na simu yake ya mkononi, huku dawa za kulevya zilizokuwa sehemu ya vielelezo zikikabidhiwa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ADU) kwa ajili ya kuteketezwa kwa mujibu wa sheria.
Jaji Otaru kwenye hukumu yake alieleza kuwa ni kanuni iliyoanzishwa kisheria kwamba wajibu wa kuthibitisha shtaka la jinai ni la upande wa mashtaka na wajibu huo lazima utekelezwe bila shaka yoyote.
Alisema kwa kujibu hilo ni lazima vipengele vinne vijibiwe ambavyo ni iwapo kilichokamatwa ni dawa za kulevya na iwapo ina uzito wa zaidi ya gramu 200, iwapo mlolongo wa ulinzi uliimarishwa, iwapo mshtakiwa alikuwa akisafirisha dawa za kulevya na iwapo upande wa utetezi uliibua shaka yoyote dhidi ya kesi ya mashtaka.
Jaji Otaru akieleza mapungufu ya upande wa mashtaka kuwa shahidi wa pili alidai kupokea taarifa kwa mtoa taarifa aliyemjulisha kuhusu mshtakiwa na Henry kuwa wanajihusisha na dawa za kulevya na kuwa wakati anahojiwa na upande wa utetezi, alieleza kuwa hakutajiwa majina ya wahusika wa biashara hiyo.
Jaji amesema, shahidi huyo alieleza kuwa mtoa taarifa alitaja wanaume wawili kutoka Nigeria bila kuwataja na kuwa mlango ulipofunguliwa na mshitakiwa, Henry alimweleza kuwa kaka yake, akimaanisha mshtakiwa, atamuonyesha zilipo dawa hizo kwa sababu ndiye aliyekuwa akitunza na kusimamia dawa hizo.
Jaji amesema mashahidi wengine ambao ni shahidi wa tatu na wa saba, wote walishuhudia kuwa walisikia Henry aliwaeleza polisi kuwa angewaonyesha ndani, lakini hawakusema kuwa mshtakiwa alikuwa akisimamia dawa hizo bali kwa sababu mshtakiwa alikuwa anajua kila kitu kiliwekwa wapi.
“Sentensi hizi hutoa maana tofauti kabisa, kujua mahali kila kitu kiko, haimaanishi kujua yaliyomo ndani yake au kusimamia mambo haya. Kwa hivyo, ushahidi wa shahidi wa tatu na wa saba hayaungi mkono yale ya shahidi wa pili kwenye kipengele hiki,” alisema Jaji.
Jaji alisema kulingana na mmiliki wa ghorofa (shahidi wa nne), mpangaji wake alikuwa Mnigeria aliyekuwa anajulikana kwa jina moja la Oliver ambaye alikuwa amelipa kodi yake hadi Aprili 19,2019 na aliamini kuwa Oliver na Henrry ni mtu mmoja.
“Shahidi wa pili hata hivyo alitoa hadithi tofauti kwa kueleza kuwa uchunguzi wake ulibaini kweli kulikuwa na mtu anayeitwa Oliver katika ghorofa hiyo, lakini tayari alikuwa ameondoka nchini na sasa yuko Msumbiji,” alisema.
Jaji aliendelea kufafanua kuwa, mshtakiwa alidai Oliver alipoondoka aliacha nyumba hiyo na gari kwa ajili ya matumizi na matunzo ya Henry ambapo pia alidai Oliver aliondoka Aprili 19,2019 siku kodi yake ilipoisha.
“Inawezekana pia kwamba shahidi wa nne, hakuona mabadiliko kwa sababu alikuwa amemwona Oliver mara moja tu. Siku hiyo alikuwa amekaa kwenye kochi sebuleni huku yeye akiwa nje kando ya mlango wa kuingilia.
“Ilikuwa ni siku aliyoileta mkataba wa upangaji wa saini yake, lakini akamwambia kuwa mkataba huo unahitaji kutafsiriwa kwa Kiingereza kwanza, kwani haelewi lugha ya Kiswahili. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya pekee shahidi huyo kumuona Oliver, “ alisema.
Jaji alieleza kwa mujibu wa shahidi huyo, waliendelea kuwasiliana na Oliver kwa njia ya simu na kwa kuwa yeye hakuwa anaelewa lugha hiyo alilazimika kumuomba binti yake amtafsirie.
“Siku moja, Oliver alipiga simu na kuzungumza kwa Kiswahili. Kwa mshangao akamuuliza aeleze kwa nini hakutumia Kiswahili tangu mwanzo? Kulingana na shahidi wa pili, tofauti na mshtakiwa au Oliver, Henry alikuwa anajua Kiswahili.
“Je, inawezekana kwamba shahidi wa nne alianza kuwasiliana na Henry badala ya Oliver? Naamini ndivyo ilivyokuwa,” alisema Jaji.
Baada ya uchambuzi zaidi wa ushahidi, Jaji alisema ushahidi wa shahidi wa pili kuhusu Henry alichodaiwa kusema kuhusu jukumu la mshtakiwa inatikiswa na ushahidi wa mashahidi wengine na ushahidi kwa jumla.
“Hatia haiwezi kutegemea ushahidi kama huo, kama ilivyoelezwa hapo awali, wajibu wa upande wa mashtaka ni kuthibitisha kesi yao bila shaka yoyote. Lakini, jukumu la mtuhumiwa wa kumsaidia Henry katika biashara ya dawa za kulevya limejaa mashaka,” alisema.
Jaji alisema ukiwa huo ndiyo ushahidi pekee uliotarajiwa kumhusisha mshtakiwa na kosa hilo, haujaweza kuthibitisha na kumtia hatiani na kuwa Mahakama inahitimisha kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza mzigo wao wa uthibitisho.