Ruwaich ataja athari za jamii kukizoea kifo

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Yuda Thadeus Ruwa’ichi ametuma ujumbe kwa Watanzania akiwataka kutokizoea kifo kwani kufanya hivyo watakuwa viumbe wa ajabu.

Ametahadharisha endapo watu watajenga mazoea dhidi ya kifo, watasababisha mauaji ya binadamu wenzao kwa mzaha.

Ametoa wito huo leo Jumamosi Septemba 27, 2025 wakati wa misa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu, Dar es Salaam  iliyoadhimishwa kumuaga  hayati Askofu Mkuu, Novatus Rugambwa, aliyefariki dunia akipatiwa matibabu mjini Roma, Italia, Septemba 16, 2025.

Mwili Askofu Mkuu, Rugambwa, aliyekuwa Balozi wa Papa nchini New Zealand ulirejeshwa nchini jana Septemba 26 na misa ya mazishi ifanyanyika Kanisa Kuu Jimboni Bukoba, Jumatatu Septemba 29, ambako atazikwa.

“Tunapoadhimisha msiba huu tusiwe na huzuni iliyopitiliza, imani yetu itufariji na kutuongoza kama walivyo mitume, hata sisi tuna mahangaiko yetu, inabidi tujipime, tujikusanye, tujitafakari tunapokabili msiba,” amesema na kuongeza:

“Kifo hakizoeleki, kamwe tusipende kuzoea kifo kwa sababu ukikizoea utakuwa kiumbe wa ajabu sana. Ukizoea kifo unaanza kumuua mwenzako kimzaha mzaha kama vile uhai wake ni wa mbuzi, kuku, lakini uhai wa binadamu yeyote una thamani kubwa machoni pa Mungu kwa hiyo, tusijiruhusu kuzoea kifo; kiendelea kubaki kama fumbo na changamoto mbele ya kila mmoja wetu.”

Wakati Askofu Mkuu Ruwa’ichi akitoa kauli hiyo, nchini Tanzania yamekuwapo matukio ya mauaji miongoni mwa wanandoa, wazazi kuua watoto na watu kujiua, yakihusishwa na matatizo ya afya ya akili.


Mathalani, mwaka 2024, kwa kipindi cha takribani miezi mitatu, gazeti la Mwananchi liliripoti matukio 16 yaliyosababisha vifo vya watu 20 kutokana na wanandoa kuuana na wazazi kuua watoto.

Mbali ya hayo, katika maadhimisho ya siku ya kuzuia kujiua duniani, Septemba 10, 2025 ilielezwa idadi ya wanaojiua nchini inaongezeka, wanaume wakiongoza.

Ilielezwa utafiti uliofanywa na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe na Jeshi la Polisi, ulionyesha vifo 1,141 vilivyotokana na kujiua vilitokea nchini kuanzia Januari mwaka 2024 hadi Juni 2025, huku wanaume wakiongoza kwa asilimia kubwa.


Mbali ya hayo, yamekuwapo matukio ya watu kuripotiwa kupotea na baadaye miili yao kupatikana wakiwa wamekufa.

Askofu Mkuu, Ruwa’ichi amesema Askofu Mkuu Rugambwa atakumbukwa kwa kazi yake ya uinjilishaji na kuhimiza mshikamano baina ya watu kwenye jamii.

New Content Item (1)


“Ni Mtanzania wa kwanza kuingizwa kwenye orodha ya wawakilishi wa Baba Mtakatifu, Balozi wa Vatican duniani. Kupitia yeye tumepewa fursa kama Kanisa la Tanzania, tunamshukuru kwa utumishi wake huu, tumuombee kwa Mungu amsamehe mapungufu yake,” amesema.

Ameeleza namna alivyowezesha ujenzi wa shule za kusaidia watoto wa masikini, hususani wasichana iliyopo Makurunge, wilayani Kisarawe mkoani Pwani kwa kushawishi viongozi wa dini kutoka nchini Korea kuja kutoa msaada Tanzania.

Amesema shule hiyo ilianzishwa na masista wa Mama Maria kutoka Korea na Japan na kwamba, nyingine ya vijana wa kiume kutoka familia masikini inajengwa mkoani Dodoma.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi amesema kumekuwapo baadhi ya matajiri wanaotaka kupeleka watoto wao katika shule hiyo inayosimamia dhana ya kuwahudumia wanyonge, jambo alilolieleza kama kufuru na unyang’anyi.

“Nilisisitize, kwa sababu kuna watu wengine ambao wana fedha za kutupa lakini wao nao wanataka kujaribu watoto wao wakasome Makurunge, hiyo ni kufuru, huko ni kuiba na huko ni kujikita mahali ambako siyo staha ya matajiri,” amesema na kuongeza:

“Fursa hii imekusudiwa kwa mabinti kutoka familia duni wasio na uwezo wa kugharamia elimu. Tuiache fursa hii iwanufaishe walengwa.”

New Content Item (1)


Amesema shule hiyo kwa sasa inahudumia zaidi ya wasichana 1,000 kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania, ambao wanasomeshwa na kulelewa bure bila ubaguzi wa kikabila au kijamii.

Askofu Mkuu Rugambwa alizaliwa Oktoba 8, 1957, katika Jimbo Katoliki la Bukoba, nchini Tanzania. Baada ya masomo na majiundo ya kikasisi, akapewa daraja takatifu ya upadre mikononi mwa hayati Askofu Nestorius Timanywa Julai 6, 1986. Akajiunga na utume wa kidiplomasia mjini Vatican Julai mosi, 1991.

Amehudumu katika balozi za Vatican, pia aliwahi kuwa Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalumu.