MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Valentino Mashaka amesema kitendo cha Simba kumtoa kwa mkopo ni fursa kwake kujipanga ili arejee katika ushindani.
Katika mahojiano na Mwanaspoti, Mashaka anasema kujipanga upya siyo kitu cha ajabu kwa mchezaji, badala yake anaweza kufanya vitu vikubwa kuliko mwanzo akisisitiza hata Ulaya inafanyika hivyo.
Baada ya kutoonyesha kiwango bora akiwa na Manchester United msimu uliopita, Rasmus Højlund amejiunga Napoli kwa mkopo na katika mchezo wake wa kwanza dhidi ya Fiorentina wikiendi iliyopita alifanikiwa kufungua akaunti ya mabao, kitu anachokitamani Mashaka.

Mashaka anasema kabla ya kwenda katika kambi ya kujiandaa na msimu wa 2025/26 ambayo Simba iliweka Misri, kocha Fadlu Davis alimkalisha chini na kumwambia hatakuwa sehemu ya kikosi hicho, na atapelekwa kwa mkopo JKT Tanzania.Ana- sema alimjenga ili atambue thamani ya muda katika mpira wa miguu na kumsisitiza kukosa nafasi ya kucheza ni kitendo kisichokuwa na afya kwake kama kijana.
“Kocha Fadlu alisema mpira wa miguu una muda na mimi bado ni kijana napaswa kucheza kwa ajili yangu mwenyewe na taifa langu. Aliniona kipaji changu ni kikubwa nikionekana naweza nikafanya vitu vikubwa inaweza ikawa ndani ama nje,” anasema Mashaka na kuongeza:
“Hata baada ya kufika Misri alikuwa ananisisitiza nijitume katika mazoezi ili nitakapojiunga na JKT Tanzania nionyeshe kiwango cha juu, hivyo haikuwa kitu kigumu kwangu na nikawa natamani nipate timu nitakayokuwa nacheza.
“Jambo la msimgi alinisisitiza ili niwe mchezaji mwenye thamani ya juu, nizingatie nidhamu ya kila kitu, bidii ya mazoezi na kujua nataka nini katika kazi yangu na kuniambia anatarajia kuyaona makubwa kwangu kwa msimu huu”.

Anasema Fadlu ni kocha anayesimama nafasi ya kaka na mzazi kwa wachezaji, lakini linapofika suala la kazi hana mchezo:
“Nakumbuka akinipa mechi ya kucheza alikuwa ananiambia hata zikiwa dakika tano ni muhimu sana kwangu kuonyesha kitu cha tofauti.”
Anasema baada ya kupewa taarifa ya kutolewa kwa mkopo alimpigia simu wakala anayemsimamia na wazazi waliompa nguvu ya kupambana na kumwaminisha kuwa ana nafasi nyingine ya kuonyesha kipaji chake.
Mashajka anasema mapro aliocheza nao Simba waliomjenga kuhusiana na kipaji ni Elie Mpanzu, Leonel Ateba na Fabrice Ngoma.
“Kitu kikubwa walichoniambia wanakiona kipaji changu ni kikubwa, ila natakiwa kubadilisha aina ya maisha nisiishi kwa mazoea. Nizingatie mazoezi ya timu na binafsi na niyafanye kwa bidii,”anasema na kuongeza:
“Kitu kingine walichonisisitiza baada ya mazoezi natakiwa kupumzika kisawasawa ili kuupa mwili wangu nguvu, kunywa maji kwa wingi, kula vizuri na kuutumia muda wangu mwingi kwa manufaa.”

Anasema kitu ambacho alikuwa anakishuhudia mara nyingi kwa Mpanzu baada ya mazoezi ya timu ni lazima afanye binafsi: “Yule jamaa siyo mtu wa kutoka anaipenda kazi yake, hivyo kuna kitu nilichojifunza kikubwa kutoka kwake.”
Mchezaji huyo anasema nafasi aliyopata kuichezea Simba imempa manufaa ndani na nje ya uwanja kitu anachosisitiza kitasalia katika kumbukumbu za maisha yake.
“Baadhi ya mafanikio ya nje ya uwanja nimejanga, nina gari, lakini katika kazi yangu mtazamo umekuwa imara kujua mchezaji mwenye thamani kubwa anatakiwa aishi vipi, afanye nini – hicho ni kitu kikubwa nilichokipata kwa makocha na wachezaji,” anasema na kuongeza:
“Kupitia Simba kuna vitu siwezi kuvifanya katika jamii maana imenipa umaarufu unaonisaidia baadhi ya huduma kuzipata kirahisi hata baada ya kujiunga na JKT mashabiki wananitumia ujumbe kunitaka nipambane bado nina nafasi ya kufanya makubwa, hivyo upendo wao siwezi kuusahau.”
Anasema wakati yupo Geita Gold alikuwa anatamani kupata timu inayoshiriki michuano ya CAF, ikaja ikatimia baada ya kujiunga na Simba msimu uliopita iliyofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
“Simba ilicheza fainali dhidi ya RS Berkane, hivyo nina medali ya michuano ya CAF. Tayari nimeitimiza ndoto yangu ingawa natamani siku nije niivae medali ya ubingwa wa CAF sijui ni lini na nitakuwa wapi, ila kila jambo linawezekana kwa kufanya bidii,” anasema.

Kwa sasa Mashaka anasema anafurahia kujiunga na JKT Tanzania anakoamini ana nafasi kubwa ya kucheza akitofautisha na Simba ambako alikosa namba mbele ya Steven Mukwala na Ateba ambao msimu uliopita walifunga mabao 13 kila mmoja, na kukiri ushindani waliomuonyesha umemjenga.