Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu mfanyabiashara Ibrahim Mbwilo, kifungo cha miaka 20 gerezani baada ya kupatikana na hatia katika makosa mawili ambayo ni kujihusisha na nyara za Serikali pamoja na kukutwa na vipande vinane vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh34 milioni, bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Hukumu hiyo imetolewa jana Ijumaa, Septemba 26, 2025 na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga, baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa na kupelekwa mahakamani hapo.
Mshtakiwa huyo anadaiwa aliruka dhamana ya mahakama hiyo kwa kushindwa kufika mahakama hapo Agosti 12, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutolewa hukumu, hali iliyosababisha mahakama hiyo kutoa hati ya kumkamata pamoja na wadhamini wake popote walipo.
Baada ya kutolewa kwa hati hiyo, Jeshi la Polisi lilianza kumtafuta na kufanikiwa kumkamata mkoani Morogoro na kisha kumrejesha Dar es Salaam ambapo jana alifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa hukumu yake.
Awali, kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, wakili wa Serikali Winniwa Kassala, aliieleza Mahakama hiyo kuwa mshtakiwa amefikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kusomewa hukumu baada ya kuruka dhamana na kisha kukamatiwa Morogoro.
“Mheshimiwa hakimu, kwa kuwa mshtakiwa amekamatwa na kuletwa mbele ya mahakama yako, upande wa mashtaka tunaomba mahakama imsomee adhabu yake ili aungane na wenzake ambao walishaanza kutumikia kifungo chao tangu Agosti 12, 2025,” alisema Wakili Kassala.
Kassala baada ya kutoa taarifa hiyo, hakimu Kiswaga alimhoji mshtakiwa sababu ya kushindwa kufika mahakamani hapo tangu Agosti 12, 2025 hadi alipokamatwa na mahojiano yalikuwa kama ifuatavyo.
Hakimu: Mshtakiwa kwa nini usiende kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kutiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na meno ya tembo?
Hakimu: Na kwa nini ulishindwa kufika mahakamani kusikiliza hukumu ya kesi yako?
Mshtakiwa: Mheshimiwa hakimu, mimi sijahusika na kesi ya meno ya tembo.
Mshtakiwa: Mimi kuna mmoja wa washtakiwa katika kesi hii ya meno ya tembo, nilikuwa namdai hela zangu ndio akanitaja, hivyo mheshimiwa hakimu mimi sihusiki na kesi hii.
Hakimu: Kwa nini hukufika siku hiyo ya hukumu?
Mshtakiwa: Nina matatizo ya kuanguka anguka.
Mshtakiwa: Siku hiyo ya Agosti 12, 2025 nikiwa najiandaa kuja mahakamani hapa, nilianguka na kupoteza fahamu kule Kigogo ninapokaa na nikaibiwa simu na hela.
Mshtakiwa: Baada ya kuibiwa simu na hela nilifika mahakamani hapa kwa kuchelewa yaani saa tisa mchana na kukuta wenzangu wameshahukumiwa.
Hakimu: Sasa mimi natekeleza adhabu iliyotolewa na Mahakama hii Agosti 12, 2025 ambayo ni kutumikia kifungo cha miaka 20 gerezani, hivyo mshtakiwa utaanza kutumikia kifungo chako kuanzia leo (jana).
“Kama nilivyoeleza, natekeleza sheria kama ilivyo na kwa kuwa adhabu yako ilishatolewa na hakimu aliyekuwa anasikiliza kesi hii, basi mshtakiwa utaanza kutekeleza adhabu ya kutumikia kifungo chako cha miaka 20 gerezani kuanzia leo” alisema hakimu Kiswaga.
Hakimu Kiswaga baada ya kutoa maelezo hayo, mshtakiwa aliwekwa chini ya ulinzi wa maofisa wa Polisi kwa ajili ya kupelekwa gerezani.
Hukumu ilivyotolewa Agosti 12, 2025
Siku hiyo, mahakama hiyo iliwahukumu washtakiwa wawili, Sadock Rulandala na Stanley Mwaryoyo, kifungo cha miaka 20 gerezani kila mmoja kwa makosa hayo mawili, huku mshtakiwa wa tatu Ibrahim Bwiro, akiruka dhamana kwa kushindwa kufika mahakamani hapo.
Pia mahakama hiyo ilitoa amri ya kutaifisha simu tatu walizokutwa nazo washtakiwa ziwe, mali ya Serikali.
Vile vile, Mahakama hiyo ilitoa amri ya kutaifisha vipande vinane vya meno ya tembo, viwe mali ya Serikali.
Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Annah Magutu, baada ya upande wa mashtaka na ule wa utetezi kufunga ushahidi wao.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Magutu alisema upande wa Jamhuri walikuwa na mashahidi sita na vielelezo mbalimbali ikiwemo vipande vinane vya meno ya tembo ambapo walithibitisha mashitaka hayo bila kuacha shaka.
Na kabla ya kutoa adhabu hiyo, wakili Kassala, aliiomba Mahakama kutoa adhabu kali iwe fundisho kwao na wengine.
Kwa upande wa Rulandala na Mwaryoyo waliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwani ni wakosaji wa mara ya kwanza pia wamekaa ndani kwa muda mrefu.
Hata hivyo, hakimu Magutu alitupilia mbali maombi ya washtakiwa hao na hivyo kukubaliana na ombi la Jamhuri na kisha kuwahukumu kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kila kosa na adhabu hiyo inakwenda kwa pamoja, hivyo watatumikia kifungo cha miaka 20 jela.