Ziara ya mgombea wa urais wa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan katika mikoa ya kanda ya kusini imeacha matumaini kufutia ahadi tano alizozitoa zinazolenga kuchagiza uchumi ya kanda hiyo.
Kwa siku sita Samia alipita katika majimbo ya mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara akiinadi ilani ya CCM na kutoa ahadi ambazo Serikali yake itazitekeleza endapo atapata ridhaa ya miaka mitano ya uongozi katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Kama ilivyo kwa wagombea wengine Samia alieleza namna atakavyotekeleza miradi itakayotoa huduma za kijamii kama elimu, afya, maji, nishati kwa lengo la kuongeza utu wa Mtanzania.

Sambamba na huduma hizo za kijamii katika mikoa ya kusini mgombea huyo alikuwa na ahadi mahususi ambazo zimelenga kubadilisha uchumi wa mikoa hiyo.
Kuifungua kanda ya kusini ilikuwa miongoni mwa ahadi za kipaumbele kwa mgombea huyo katika mikutano yote aliyofanya kwenye mikoa hiyo kwa kile alicholeza kuwa lengo ni kuchangamsha uchumi na kuiunganisha Tanzania na nchi jirani za Malawi na Msumbiji.
Ufunguaji wa kanda ya kusini unahusisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege, bandari, miundombinu wa barabara na reli itakayotoka Mtwara hadi Mbamba Bay.
Mgombea huyo alieleza mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa ya kilomita 1,000 inayotarajiwa kupita maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa mazao ya nafaka na kuunganisha maeneo ya kiuchumi ya Liganga na Mchuchuma.

Kwenye viwanja vya ndege ahadi ilikuwa kuendeleza ujenzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege vya Mtwara na Songea huku ukielezwa mpango wa kujengwa uwanja wa ndege wa Lindi.
Uanzishwaji kongani za viwanda
Kila alikopita mgombea huyo aliahidi kuanzishwa kwa kongani za viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na madini yanayopatikana katika eneo husika.
Akiwa katika mikoa hiyo ameahidi viwanda vya kuongeza thamani ya samaki na dagaa wanaovuliwa ziwa Nyasa, kuongeza thamani kahawa, korosho, ufuta, mbaazi na mazao mengine yanayozalishwa katika mikoa ya kusini.
“Hatutaki kuona korosho zetu zikiuzwa ghafi na faida kubwa ikaenda nje ya nchi. Tunataka mnyororo mzima wa thamani ukae hapa kwetu kuanzia uzalishaji, uchakataji, hadi usafirishaji. Hii italeta ajira, kipato kwa wakulima na mapato kwa serikali,” alisema .
Uendelezaji wa zao la korosho
Mgombea huyo aliahidi kuendeleza mapinduzi katika sekta ya kilimo, akisisitiza kuwa Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa katika ruzuku ya pembejeo ili kuongeza uzalishaji, hasa wa korosho katika mikoa ya kusini.

Pia, aliahidi kuendeleza utoaji wa dawa kwa ajili ya kuua wadudu wanaoshambulia zao hilo lengo likiwa ni kuongeza uzalishaji na kuifanya korosho ya Tanzania kuendelea kupamba thamani barani Afrika.
Ahadi nyingine ni kuimarisha vyama vya ushirika ambavyo kwa muda mrefu vimekuwa vikikabiliwa na changamoto za ubadhirifu wa fedha na ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima.
Kuongeza tija kwenye kilimo
Alisema endapo atapa ridhaa ya kuongeza miaka mitano mingine itahakikisha bei za mazao ya wakulima wa mkoa huo zinapanda, hasa kwa mazao wanayoyategemea zaidi kama korosho, mbaazi, ufuta na karanga.
Samia amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka Serikali imetumia Sh726 bilioni kugharamia mbolea na pembejeo za ruzuku kwa wakulima nchini, wastani wa Sh152 bilioni kwa mwaka.
Pembejeo hizo zinatajwa kuongeza mazao yanayozalishwa katika mikoa ya kusini hivyo itaendeleza jitihada hizo.

Ahadi nyingine katika eneo hilo ni kutengeneza skimu za umwagiliaji ili wakulima walime mara mbili kwa mwaka.
Kuanza mradi wa gesi asilia
Ahadi nyingine iliyokonga nyoyo za wakazi wa mikoa ya kusini ni kuanza kwa kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa gesi asilia katika kijiji cha Likong’o Mchinga.
Akihutubia katika kampeni zake mkoani Lindi Samia alisema Serikali ipo katika hatua za mwisho za makubaliano kabla ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ambao uwekezaji wake unagharimu dola za Marekani 40 bilioni.
“Sisi pia tunaoletewa mradi ni lazima tuwe na uhakika utatuletea nini na maliasili yetu inayokwenda kutumika. Kwa maana hiyo tumekuwa na mizunguko ya mazungumzo, tumezungumza sana kwa miaka miwili sasa tunakaribia kukubaliana,” alisema.