Dar es Salaam. Jana, Ijumaa, Septemba 26, 2025, Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma ilimpa kibali, Luhaga Mpina, kufungua shauri kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uteuzi wake wa kuwa mgombea urais kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.
Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Wilbert Chuma, ameelekeza Mpina kufungua shauri hilo ndani ya siku 14, kuanzia tarehe ya uamuzi huo (Septemba 26).
Mpina amepata kibali hicho baada ya kuvuka kiunzi cha kwanza cha pingamizi la awali lililowekwa dhidi ya shauri lake la maombi.
Katika pingamizi, wajibu maombi ambao ni Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) waliibua hoja tatu.
Mosi, kwamba maombi hayo ni matumizi mabaya ya taratibu za mahakama na yamepitwa na wakati, kwani yanakusudia kufuta na kukwepa kwa njia isiyo sahihi athari za kisheria za uamuzi wa Septemba 15, 2025 wa chombo cha kikatiba na kisheria chenye mamlaka ya kipekee (Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi -INEC), ambacho kiliamua na kuhitimisha uteuzi wa mwombaji wa kwanza (Mpina) kugombea urais.
Pili, kwamba maombi hayo ni batili kisheria kwa kuwa hayafai kuletwa kwa njia ya mapitio ya kimahakama na tatu, kwamba kiapo cha kuunga mkono maombi hayo kina dosari zisizorekebishika kwa kukiuka masharti ya amri ya XIX Kanuni ya 3 ya Sheria ya Mwenendo wa Madai.
Hata hivyo, mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake ilitupilia mbali hoja zote za pingamizi hilo ikieleza hazina mashiko. Imekubali hoja za Mpina na mawakili wake.
Kisha mahakama katika kuamua maombi ya msingi imekubali hoja za Mpina kupitia mawakili wake, John Seka na Edson Kilatu kuwa amekidhi vigezo vyote vya kisheria kuruhusiwa kufungua shauri la Mapitio ya Mahakama kupinga uamuzi wa Msajili.
Uamuzi huo ni mwendelezo wa anayokabiliana nayo Mpina katika kupambana na kupangua vikwazo vinavyozunguka safari yake ya kuelekea sanduku la kura za urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025. Vikwazo vinaifanya njia anayopita kuelekea sanduku hilo kuzidi kuwa nyembamba.
Mpina alipitishwa na Mkutano Mkuu wa ACT-Wazalendo, Agosti 6, 2025 kuomba uteuzi wa INEC kupeperusha bendera yake katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, Agosti 26, Msajili wa Vyama vya Siasa, alitangaza kubatilisha uteuzi wake kutokana na pingamizi lililowasilishwa kwake na aliyekuwa Katibu Mwenezi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam, Monalisa Ndala.
Alidai uteuzi wa Mpina ni batili kwani hakuwa na sifa kwa mujibu Kanuni za Kudumu za Uendeshaji wa chama hicho, Toleo la mwaka 2015.
Monalisa alidai Mpina anakosa sifa zote hizo, kwa kuwa alijiunga na chama hicho, Agosti 5, 2025 na aliteuliwa siku moja baada ya kujiunga badala ya siku 30 kabla.
Kutokana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, INEC ilitangaza kumuondoa Mpina katika orodha ya walioomba kuteuliwa kugombea nafasi hizo katika uchaguzi huo.
Vilevile, INEC ilimtaka Mpina asifike ofisi zake siku ya uteuzi wa wagombea, Agosti 27, 2025 na hata alipokwenda alizuiwa na askari polisi kuingia katia ofisi hizo.
Mpina alianza mapambano ya kisheria, kuanzia tarehe hiyohiyo aliyozuiwa kuingia ofisi za INEC kurejesha fomu yake, kwa kufungua mashauri mawili mahakamani.
Shauri la kwanza lilikuwa la Kikatiba lililofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo (mwombaji wa kwanza) na Mpina (mwombaji wa pili) dhidi ya INEC na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika shauri hilo namba 21692 la mwaka 2025 lililofunguliwa chini ya hati ya dharura, pamoja na mambo mengine walipinga uamuzi wa INEC kumuengua Mpina katika orodha ya wagombea walioomba uteuzi wake kutoka vyama mbalimbali.
Pia, walifungua shauri dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Katika shauri hilo la maombi namba 23617 la mwaka 2025, Mpina na Bodi ya Wadhamini wa ACT-Wazalendo (mwobaji wa kwanza na wa pili mtawalia) waliomba kibali cha kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga uamuzi wa Msajili kubatilisha uteuzi wake.
Katika uamuzi uliotolewa Septemba 11, 2025 na jopo la majaji watatu, Abdi Kagomba (kiongozi wa jopo), Evaristo Longopa na John Kahyoza, mahakama ilitengua uamuzi wa INEC.
Mahakama ilifikia uamuzi huo baada ya kukubali hoja za Mpina kwamba hakupewa haki ya kusikilizwa na INEC wakati ilipomuengua, kinyume cha Ibara ya 13(6) (a) ya Katiba ya Nchi.
Hivyo, mahakama ilibatilisha uamuzi wa INEC kumuengua Mpina na kuiamuru ipokee fomu zake za kuomba utezi na iendelee na mchakato wa uteuzi wake kuanzia pale ulipokuwa umeishia.
Baada ya mahakama kutoa uamuzi huo, Mpina alijikuta akikabiliwa na kikwazo kingine cha pingamizi tatu kuhusu uteuzi wake zilizowekwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mgombea urais wa Chama cha AAFP na mgombea urais wa Chama cha NRA.
Licha ya kuwapo pingamizi hizo, Septemba 13, 2025 INEC kwa kuzingatia uamuzi wa mahakama ilipokea fomu za Mpina na baada ya kuzikagua na kujiridhisha kuwa zilikuwa sawa, ilimteua kuwa mgombea wa urais kupitia ACT- Wazalendo.
Furaha ya Mpina kuvuka kizingiti hicho haikudumu, kwani hata kabla ya kuzindua kampeni, ikiwa ni siku moja tu baada ya kuteuliwa, alijikuta nje ya mbio za kuusaka urais baada ya uteuzi wake kutenguliwa tena na INEC.
Katika uamuzi wake wa Septemba 15, 2025, INEC ilitupilia mbali pingamizi za wagombea wa AAFP na NRA dhidi ya Mpina, lakini ikakubali la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo ikatengua tena uteuzi wake.
Uamuzi huo ulisababisha Mpina na Bodi ya Wadhamini ya ACT- Wazalendo kuirudisha INEC mahakamani kwa mara nyingine ambako wamefungua shauri la kikatiba dhidi yake Tume na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupinga uamuzi huo.
Katika shauri hilo pamoja na mambo mengine wanadai INEC haikuzingatia sheria na Katiba ya Nchi kutathimi sifa za mgombea.
Badala yake wanadai INEC ilizingatia uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, na hasa mambo yanayohusu migogoro ya ndani ya chama kati ya wanachama ambayo si miongoni mwa vigezo vya kisheria vya sifa za mgombea.
Hivyo, Mpina bado ana safari ya kupangua vikwazo vilivyo mbele yake kabla ya kushiriki kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.