CRDB yafungua tawi jipya Namanga, kuchochea biashara mipakani

Arusha. Benki ya CRDB imefungua rasmi tawi jipya katika mpaka wa Namanga kwa ajili ya kutoa huduma, hatua inayolenga kuongeza ujumuishi wa kifedha na kuchochea biashara katika mpaka huo kati ya Tanzania na Kenya.

Uzinduzi wa tawi hilo, unafanya benki ya CRDB kufikisha jumla ya matawi 268 nchini.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi Wilayani Longido, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na Tehama ili kurahisisha mawasiliano na kuvutia uwekezaji zaidi nchini, hasa huduma za kifedha ili ziwafikie wananchi.

Pia amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha huduma za kifedha zinakuwa nguzo ya maendeleo ya taifa, sambamba na malengo ya kufikia uchumi wenye thamani ya dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.

“Huduma za kifedha siyo tu benki, bali ndiyo msingi wa ustawi wa kaya, ukuaji wa biashara na ustahimilivu wa taifa kiuchumi,” amesema Makalla na kuongeza;

“Kupitia upanuzi wa huduma kama huu, wananchi wa maeneo ya mipakani wataweza kupata mitaji, kuweka akiba salama na kushiriki kikamilifu katika biashara za kikanda.”

Makalla amesema uwepo wa CRDB Namanga ni ishara ya kuimarika kwa uchumi jumuishi katika maeneo ya mipakani.

“Tawi hili litaongeza kasi ya biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa wateja wadogo na wa kati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul, amesema uamuzi wa kufungua tawi jipya Namanga ulitokana na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za kifedha kutokana na kuimarika kwa biashara mipakani.

Mkurugenzi wa wateja wadogo na wa kati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul, akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Tawi la benki ya CRDB eneo la Namanga



“Hapo awali tulihudumia jamii kupitia gari la kibenki linalotembea, lakini mahitaji yamekua zaidi ya uwezo huo”.

“Tawi hili jipya litawezesha wafanyabiashara kupata huduma kwa urahisi na kuongeza kasi ya biashara mipakani,” amesema Paul.

Kwa sasa CRDB inamiliki jumla ya matawi 268 nchini, ikilinganishwa na matawi 19 pekee ilipoanzishwa mwaka 1996.

Hatua hii inakuja wakati benki hiyo ikisherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwake, huku ikiwa katika mchakato wa kupanua huduma zake kimataifa kuanzia na Dubai, baada ya kuingia Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mbali na hilo, benki hiyo imefanikiwa kutoa mikopo ya zaidi ya Sh10 bilioni kwa vikundi visivyo rasmi, hatua inayochochea ujumuishi wa kifedha na kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi.

Wakazi wa Wilaya ya Longido wanaofanya biashara katika eneo la mpaka huo wa Namanga wamesema kuwa wanafurahishwa na huduma mpya, wakisema itawaondolea changamoto za muda mrefu za kifedha.

“Hii ni faraja kubwa kwa wafanyabiashara kama sisi. Tutaweza kuweka akiba kwa usalama, kupata mikopo kwa urahisi na kuendesha biashara zetu bila vikwazo tulivyokuwa tukivipitia awali,” amesema Neema Laizer, mfanyabiashara wa eneo hilo.

Ametumia nafasi hiyo kuiomba Serikali kuimarisha huduma ya mawasiliano ili kurahisisha miamala ya kifedha Kupitia simu zao.

Steven Mollel amesema kuwa ufunguzi wa tawi la Namanga unakwenda sambamba na mikakati ya kuimarisha ujumuishaji wa kifedha na biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Kwa kuwekeza katika maeneo ya mipakani, CRDB siyo tu kwamba inafungua fursa mpya za kibiashara, bali pia inachangia kujenga uchumi wa kikanda wenye ustahimilivu na jumuishi hivyo tunawapongeza sana,” amesema Mollel