Moshi. Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema kuwa chama hicho kitalitazama kwa karibu kundi la vijana, kulijengea mazingira mazuri ya uchumi na ajira kuanzania kwenye halmashauri.
Wasira amesema hayo alipokuwa akizungumza na wana CCM mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kuhusu kufanikisha ushindi wa kishindo kwa chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu.
Amesema Serikali chini ya CCM imeboresha sera ya elimu kutoa fursa kwa wanafunzi kuanzia shule za sekondari kuwa na ujuzi mbalimbali ambao utawasaidia kujikwamua kiuchumi.
Amesema kupitia mfumo mpya wa elimu vijana watapata ujuzi wakiwa shule za sekondari na vyuo vya ufundi stadi (Veta).

“Tunabadili mfumo wa elimu ili vijana wetu wanaosoma sekondari wakitoka wawe wana ujuzi, wawe wanajua umeme, wawe wanajua mabomba ya maji yakikatika yanaungwa vipi, tunataka wawe wanajua kama ni biashara, biashara gani wanaweza kufanya na ikawalipa tunawapa elimu ya ujuzi.
“Ujuzi mwingine anaupata sekondari katika vyuo vya Veta, ndiyo maana ilani inatutaka kujenga vyuo hivyo kila wilaya na kila halmashauri ili vijana wetu wasiwe na wasiwasi, wasitembee wanatafuta kazi.”
“Tumekubaliana katika ilani vijana wasomi waanzishe kampuni wanaita ‘start-up’ na tumesema lazima wapewe mikopo ya zana ili wajifanyie kazi zao wenyewe. South Korea (Korea Kusini) ndivyo walivyofanya na wameendelea kwa kutumia ‘brain’ (akili) na nyinyi hapa Moshi brain iko nyingi tu mnaweza mkaunda kampuni na mkasaidiwa mikopo na zana na mkafanya kazi nyingi ambazo Serikali inazifanya sasa.
“Mkapewa tenda kama ni barabara mkatengeneza, tunataka kampuni ‘local’ (za ndani) siyo kila barabara hata ya kilomita mbili tuwape wageni. Tunataka wachimbe visima vya maji, waunganishe mabomba, watengeneze barabara za lami fupifupi ambazo katika ilani hii Moshi inatakiwa kuwa na barabara nzuri za mitaani. Hayo ndiyo mambo tunayoyaahidi,” ameeleza.

Kuhusu amani Wazira amesema, “Chama cha Mapinduzi kitasimama na mataifa yote yanayopenda amani duniani, sisi tunataka amani iwe ndiyo msingi wa maendeleo yetu.
“Mtu yeyote katika Tanzania awe ndani au nje ya Tanzania anayetaka tuige siasa za chuki tunamwambia atusamehe hakuna nafasi ya kuvunja amani ya Tanzania,” amesema.
Amesema CCM miongoni mwa majukumu iliyorithi kutoka kwa vyama vya ukombozi Tanu na Afro Shiraz ni kuhakikisha inawaletea maendeleo Watanzania.
“Jambo lingine ambalo CCM imelirithi kutoka kwa vyama vya Afro Shiraz na Tanu ni maendeleo ya watu, tunataka maendeleo ya watu na maendeleo tunayatamka kila baada ya miaka mitano katika ilani, Watanzania tunawaahidi tutafanya moja, mbili, tatu, nne.
“Baada ya miaka mitano tunarudi tunawaambia tumefanya moja, mbili, tatu, nne. Tupeni ridhaa kwa sababu tutafanya moja, mbili, tatu, nne tano.
“Hatuji hapa kutafuta dola kwa nguvu, tunatafuta dola kutoka kwa Watanzania kwa njia ya kura,” amesisitiza.