NAHODHA wa Mashujaa FC, Baraka Mtuwi amesema wapo tayari kuikabili Singida Black Stars aliyoitaja kuwa haitakuwa rahisi kutokana na uwepo wa nyota wengi bora.
Mashujaa inatarajia kushuka dimbani Jumanne ya wiki ijayo, kwenye Uwanja wa KMC kucheza mechi ya tatu ya Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare moja.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mtuwi alisema wataingia kwa kuiheshimu Singida Black Stars ambayo ameitaja kuwa ni bora kutokana na uwepo wa nyota wengi wa kigeni na wazoefu.
“Tutaingia kwa kuiheshimu Singida kwani ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri lakini na sisi tupo vizuri tumejiandaa kwa ajili ya kushindana, matarajio yetu ni kukusanya pointi tatu.
“Kikosi chetu hakina mabadiliko mengi licha ya ongezeko la wachezaji ambao wanaendelea kujitafuta kuingia kwenye mfumo, mambo yanaenda vizuri tunatarajia kufanya mambo makubwa msimu huu,” alisema Mtuwi.
Akizungumzia ubora wa timu yao, alisema sasa wanajitafuta lakini wana timu bora na ya ushindani kutokana na maingizo mapya ambayo yalizingatia mahitaji ya timu hiyo kwa msimu uliopita.
“Kocha amesajili maeneo ambayo aliona kulikuwa na upungufu, hajafanya usajili ilimradi ajaze mapengo, ameongeza wachezaji bora ambao wameongeza changamoto ya namba na ubora wa timu, hivyo tunatarajia msimu bora kutokana na ubora wa kikosi.”
Mashujaa imeanza ligi msimu huu kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya JKT Tanzania kisha ikaibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, mechi zote ilicheza uwanja wake wa nyumbani Lake Tanganyika mkoani Kigoma.
Nahodha Mashujaa kaahidi jambo | Mwanaspoti
