Manyama ajiweka sawa Azam | Mwanaspoti

BEKI wa kushoto wa Azam FC, Edward Manyama amesema kwa namna Ligi Kuu Bara msimu huu ilivyoanza kwa ugumu, inampa picha ya namna anavyotakiwa kukaza buti kuhakikisha huduma yake inakuwa muhimu kikosini.
Manyama aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali kama JKT Ruvu, Yanga, Ruvu Shooting, Namungo na Singida Black Stars, alisema ushindani wa ligi umekuwa ukiongezeka msimu hadi msimu, kama mchezaji anachozingatia ni mazoezi ya ufiti.
“Azam kwa msimu huu inacheza Kombe la Shirikisho, kuna mechi za Ligi Kuu na FA, ili kucheza kwa kiwango muda wote ni kujituma katika mazoezi na kulinda kiwango kitakachokuwa msaada kwa timu. “Kuna ushindani wa namba unaonifanya nijitume kwa bidii kuhakikisha napata nafasi ya kucheza, ili kuonyesha ufundi na kipaji changu,” alisema Manyama.
Katika nafasi anayocheza Manyama ambayo ni beki wa kushoto na kati, anawania nafasi na wachezaji kama Pascal Msindo aliyeanza dhidi ya Al Merriekh Bentiu, Yoro Diaby na Landry Zouzou.