BAADA ya beki wa KVZ, Juma Hassan Shaaban maarufu James kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu akikosekana katika maandalizi ya timu hiyo kwa ajili ya msimu mpya wa Ligi Kuu Zanzibar, hatimaye amerejea huku akiwapiga mkwara wapinzani wao.
Mwanaspoti limemshuhudia James akiwa mazoezini na kikosi cha KVZ ambapo alisema kurejea kwake kikosini, timu hiyo ipo salama na ataipambania kwa hali zote kuhakikisha inafanya vizuri msimu huu, hivyo wapinzani wajipange.
Alisema nguvu na mbinu zote zitaanzia katika mechi ya kwanza dhidi ya JKU ambayo itachezwa Oktoba Mosi 2025 kwenye Uwanja wa Mao A uliopo Unguja, saa 10:15 jioni.
“Nafahamu haitakuwa mechi rahisi kwa sababu hata timu ya JKU ina wachezaji wazuri, lakini tutapambana ili kuanza ligi vizuri,” alisema James.
Mbali na hilo, beki huyo alisema kwa sasa anatamani kuichezea Ligi Kuu Bara na anaamini malengo yake yatatimia zaidi akiwa ndani ya ligi hiyo yenye nafasi na fursa kwa wachezaji wengi.
“Siwezi kuibeza Ligi ya Zanzibar lakini bado ipo chini ikilinganishwa na Tanzania Bara, nina uhakika nikipata nafasi ya kuichezea ligi hiyo malengo yangu yatatimia,” alisema James.
James arejea KVZ, apiga mkwara mzito
