Mavunde kuanzisha klabu za wazee jimboni Mtumba

Dodoma. Mgombea ubunge wa Jimbo la Mtumba (CCM),  Anthony Mavunde amejifunga katika mambo 10 akihutubia wananchi katika Kata ya Nghong’ona huku akielekeza nguvu kuanzisha klabu za wazee.

Katika mkutano huo, Mavunde amesema ni wakati sasa kuwakumbuka wazee na kuwaanzishia klabu zao ili tuwaweke pamoja na kusikiliza matatizo na changamoto zinazowakabili.

“Jimbo lilikuwa na Kata 41, lakini tulifanya vizuri, leo tunakuwa na kata 20 naamini tutafanya vizuri zaidi, nikopesheni imani yenu ili nikawalipe uaminifu wangu, tutajenga Miundombinu, vituo vya afya lakini tutajenga stendi ya daladala,” amesema Mavunde.

Ahadi nyingine alizotoa mgombea huyo ni kusimamia miradi mikubwa ambayo imefanyika ndani ya kata hiyo ikiwemo sekta ya afya, elimu, maji, barabara na nishati.

Ametaja ukamilishwaji na kusajiliwa Shule ya Sekondari Mapinduzi, upimaji wa ardhi, uchimbaji kisima na kuongeza kina cha bwawa la umwagiliaji na ujenzi wa soko.

Mavunde amewaomba wananchi kumpa kura za kishindo mgombea wa kiti cha Rais kwa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni Samia Suluhu Hassan na diwani wa kata anayegombea kwa chama hicho tawala.

Katika hatua nyingine ameahidi kumaliza tatizo la ufunguzi wa barabara kwa kununua mtambo (Motor Grader) kwa ajili ya Jimbo la Mtumba ili kusafisha na kufungua barabara katika maeneo yote.

Kata ya Nghong’ona ndipo kilipo Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) na Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa lakini barabarani za ndani hazijafunguka na baadhi ya maeneo bado kuna changamoto ya upungufu wa maji.