Tahadhari zachukuliwa vifo vya samaki Mto Malagarasi

Dar/Kigoma. Serikali mkoani Kigoma imesema wananchi wanaendelea kupata huduma ya maji kwa matumizi ya nyumbani kutoka vyanzo vingine salama, huku uchunguzi wa kitaalamu ukiendelea kufanywa kuhusu vifo vya samaki na viumbe wengine vilivyogunduliwa ndani ya Mto Malagarasi.

Wananchi ambao wamekuwa wakipata maji kwa matumizi mbalimbali kutokana na chanzo hicho, wameacha kuyatumia kutokana na  tahadhari iliyotolewa na serikali kwa kushirikiana na wataalamu ili kupisha uchunguzi wa nini chanzo cha vifo vya viumbe hivyo ili kuepuka madhara kwa  binadamu.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumamosi Septemba 27, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, amesema wananchi wanaendelea kutumia maji kutoka vyanzo vingine salama.

Amesema serikali inafuatilia kuona kama kuna haja ya kuongeza huduma za ziada ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa jamii hiyo.

“Maji ya Mto Malagarasi hauwezi kuyatumia, vivyo hivyo kama yalivyo hata bila ya tatizo lililojitokeza. Hata hivyo, kwa sasa wananchi wa maeneo hayo wanapata maji kutoka vyanzo vingine kwa kuwa vipo katika eneo hilo tofauti na Mto Malagarasi,” amesema.

Balozi Sirro amesema serikali inafuatilia kwa karibu kubaini na kuchukua hatua za haraka kama kuna uhitaji kwa lengo la kuhakikisha wananchi hawakosi huduma muhimu za maji wakati uchunguzi wa sababu za tukio hilo ukiendelea.

Tayari kamati maalumu ya uchunguzi imeundwa ikijumuisha wataalamu mbalimbali na imeshaanza kazi kwa kuchukua sampuli za viumbe waliokufa ili kubaini chanzo cha tatizo na kama kuna madhara ya kibinadamu ili kutatua tatizo hilo.

Wiki hii wakazi wa Kijiji cha Kigadye, wilayani Kasulu, walishuhudia idadi kubwa ya samaki wakiwa wamekufa na kuelea juu ya maji ya Mto Malagarasi, hali iliyozua taharuki na hofu kwa jamii inayotegemea mto huo kwa chakula na maji.

Baadhi ya wananchi walisema hawajawahi kushuhudia tukio la aina hiyo kwa miongo kadhaa, huku wakiendelea kunufaika na fursa mbalimbali za mto huo, zikiwamo upatikanaji wa maji kwa matumizi kadhaa yakiwamo ya kilimo, majumbani na vitoweo.

Baada ya tukio hilo, serikali ilitoa tamko ikiwataka wananchi kuacha kuvua samaki au kutumia maji ya Mto Malagarasi hadi uchunguzi utakapokamilika.

Hatua hiyo ililenga kulinda afya za wananchi na kuzuia madhara yoyote ya kiafya endapo chanzo cha vifo vya samaki kingekuwa ni sumu au uchafuzi wa maji.

Ofisa Usafi na Mazingira Mkoa wa Kigoma, Nesphory Sugu alisema kwa kushirikiana na wataalamu wa afya, sampuli ya maji katika mto huo ilichukuliwa kwa ajili ya uchunguzi.

Mganga Mkuu wa mkoa wa huo, Dk Damas Kayere, alisema hakuna mtu aliyepata madhara kutokana na tukio hilo, bali ametoa wito kwa wananchi wa eneo hilo kufika kwenye vituo vya afya iwapo watapata athari zozote kutokana na kutumia maji au kula samaki wa mto huo.

“Afya ya wananchi wetu ndiyo kipaumbele cha kwanza. Hivyo, tunawataka wananchi wote wa maeneo yanayopitiwa na mto huu kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu,” amesema Balozi Sirro alipotembelea eneo hilo kuona kilichotokea.

Umuhimu wa Mto Malagarasi

Mto Malagarasi ni mrefu na wa pili kwa ukubwa nchini Tanzania baada ya Mto Rufiji. Una mchango mkubwa kiikolojia na kiuchumi si tu kwa Kigoma, bali pia kwa Taifa, ukitoa maji kwa vijiji vingi vya Kigoma na Tabora na kuchangia katika Bonde la Ziwa Tanganyika. Pia, ni makazi ya samaki aina mbalimbali ambao wamekuwa tegemeo la lishe na kipato cha wakazi wa Kigoma.

Kwa sababu hiyo, tukio la samaki kufa kwa wingi limekuwa na athari kubwa si tu kwa mazingira, bali pia kwa uchumi mdogo wa kaya.

Kwa sasa kinachosubiriwa ni kamati ya uchunguzi ambayo matokeo yake yatatoa mwanga juu ya chanzo cha tatizo hilo na hatua sahihi za kuchukua ili kuendelea kunufaika na fursa za mto huo.