Mwanza. Kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) kilichopo jijini Mwanza, kimefanikiwa kukusanya tani tano za madini ya dhahabu kwa kipindi cha mwaka mmoja, na kuendelea kuipaisha Tanzania katika sekta ya madini kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza leo Septemba 27, 2025 na ujumbe kutoka Malawi, Ofisa Madini kutoka mkoani Mwanza Mhandisi Nyaisara Mgaya, ameeleza ujio huo umetembelea kwa lengo la kujifunza kuhusu usimamizi na uendeshaji wa biashara ya madini, hususan mfumo wa masoko unaotumika nchini Tanzania.
“Kiwanda hiki kina uwezo wa kusafisha hadi kilo 960 za dhahabu kwa siku, ingawa kwa sasa kinatumia mashine zenye uwezo wa kusafisha kilo 480 kwa siku, kutokana na upatikanaji wa malighafi pia tumefanyikiwa kukusanya tani tano za dhahabu kwa kipindi cha tangu BoT ilipoanza kununua,” amesema Mgaya.
Aidha, kiongozi wa ujumbe kutoka Malawi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Maendeleo ya Biashara za Vikundi nchini humo, Zizwan Khonje amemshukuru Ofisa Madini wa Mkoa wa Mwanza kwa elimu waliyoipata kuhusu mfumo wa biashara na masoko ya madini hapa nchini.
“Tanzania ni mfano wa kuigwa katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na hatua mbalimbali ilizochukua katika kuboresha sekta ya madini, ikiwemo uanzishwaji wa masoko ya madini ya wazi na matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa rasilimali,” amesema Khonje.
Ziara hiyo ya ujumbe kutoka Malawi inatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya madini ya nchi hiyo kwa kuimarisha mifumo ya uwazi, kuongeza mapato ya serikali na kuwezesha ushirikishwaji wa wachimbaji wadogo kwenye soko la kimataifa la madini.
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza rasmi kununua dhahabu kutoka kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu, Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR) Oktoba 01, 2024.