Singida BS yapeta CAF ikiitandika Rayon Sports

WANA fainali ya Kombe la FA msimu uliopita, Singida Black Stars, imefuzu hatua ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitandika Rayon Sports ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1.

Ushindi huo umetokana na leo Singida Black Stars kushinda mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam ikiwa ni mechi ya marudiano baada ya ile ya ugenini iliyofanyika wiki iliyopita nchini Rwanda, kushinda 1-0.

Mabao ya mchezo wa leo upande wa Singida Black Stars yamefungwa na Idriss Diomande dakika ya 44 na Antony Tra BI dakika ya 57.


Ingawa Singida BS ilitanguliwa kwa bao la kwanza na kufanya wapinzani kuweka mzani sawa pale Rayon Sports ilipofunga kupitia Gloire Tambwe dakika ya 38, lakini ilionekana kucheza vizuri hadi iliposawazisha na kwenda mapumziko matokeo yakiwa 1-1, kisha kumaliza kazi kipindi cha pili.

Kikosi cha Singida BS ambacho kipo chini ya kocha Miguel Gamondi aliyeifikisha Yanga kucheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-2024 na kucheza makundi ya michuano hiyo 2024-2025, kilionyesha kiwango bora na nidhamu kuanzia kwenye eneo la kuzuia hadi kushambulia.


Hata hivyo, ndani ya kikosi hicho uwepo wa wachezaji wenye uzoefu kama Clatous Chama, Khalid Aucho na wengineo kiliipa uhai timu hiyo ambayo ilionyesha juhudi ya kuitaka mechi kuanzia filimbi ya kwanza hadi mwisho.