Furaha ya wazazi inayoangamiza kesho ya watoto

Dar es Salaam. “Mitandao haisahau.” Ni usemi kueleza kwamba, lolote liwekwalo mtandaoni, ama iwe ni picha, maandiko, video, maoni au taarifa binafsi hubaki na kuna uwezekano wa kuonekana hata kama likifutwa.

Hii ni kutokana na kuwa, taarifa mara nyingi huhifadhiwa kwenye seva mbalimbali, watu huhifadhi kwa kuzipakua au kuzipiga picha na wana uwezo wa kuzisambaza tena.

Mitandao mingi huendelea kuhifadhi kumbukumbu kwa sababu za kisheria au kibiashara, hivyo kabla ya kuchapisha jambo mtandaoni ni muhimu kufikiria athari zake kwa muda mrefu.

Licha ya ukweli huo, katika miaka ya hivi karibuni ambayo matumizi ya mitandao yameshika kasi baadhi ya watu wakiwamo wazazi na walezi wamekuwa wakipakia mtandaoni maudhui mbalimbali yakiwahusisha watoto.

Baadhi ya maudhui hayo yanalenga kuelimisha lakini yapo pia yanayokiuka maadili, sheria na miongozo inayolinda ustawi wa watoto.

Baadhi wamekuwa wakipakia mitandaoni picha na video zilionyesha watoto wakishiriki mashindano ya muziki unaochezwa katika namna isiyo na staha.

Hivi karibuni video iliyomuonyesha mama akimnywesha pombe mtoto iliibua mjadala, jamii ikionywa kujiepusha na vitendo vya namna hiyo.

Matendo ya namna hiyo yanakiuka Sheria ya Mtoto Sura ya 13 na Urekebu wa mwaka 2023 kifungu cha 9(3) na 13 ikisomwa kwa pamoja na Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 na Urekebu wa mwaka 2023 kifungu cha 169A.

Licha ya kukiuka sheria, wataalamu wa malezi wanabainisha matendo hayo yana athari hata katika malezi na makuzi ya mtoto.

Akizungumza na Mwananchi, Irene Fugara, mtaalamu wa malezi kutoka shirika linaloshughulikia masuala ya watoto na malezi la Bright Jamii Initiative, anatoa mfano wa ‘challenge’ za mitandaoni ambazo baadhi ya wazazi hufanya na watoto.

Anasema zinapokuwa na maudhui hasi kwa mtoto huweza kumuathiri kimaadili na kisaikolojia.

Vilevile, anasema zinaweza kusababisha athari katika afya ya mwili na ya akili ya mtoto.

Irene ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo anasema baadhi ya mashindano hayo yaliyozoeleka kuitwa challenge yanaweza kuwapotosha watoto kimaadili, kwa kuwa yanahusisha lugha chafu, mavazi yasiyofaa au tabia zisizokubalika kijamii.

“Mfano mzazi anajirekodi akiwa na mtoto wakicheza muziki kwa mitindo isiyo na maadili, au wakiwa wamevaa nguo kinyume cha maadili hii siyo sawa kwa malezi na makuzi ya mtoto,” anasema.

Anaeleza kufanya hivyo kunaweza kumweka mtoto katika hatari ya kukua akiwa na msongo wa mawazo.

“Kama tujuavyo teknolojia haisahau, video hiyo inaweza kutumika baadaye na watu wenye nia ya kumdhalilisha, hivyo kumsababishia mtoto kuendelea kukua huku akiwa na majuto juu ya kile kilichorekodiwa,” anasema.

Anasema msongo wa mawazo na majuto huweza kumuweka katika hatari ya kupata matatizo ya afya ya akili.

Anasisitiza kama ikilazimika mtu kuweka picha au video ya mtoto anatakiwa kuhakikisha ina maudhui chanya kwa mtoto na kwa jamii.

Kwa upande wake, Victor Mukiza, ofisa miradi wa shirika linaloshughulika na masuala ya ulinzi wa mtoto la Save the Children, anasema vitendo vya namna hiyo ni udhalilishaji kwa mujibu wa sheria ya mtoto, kwani vinatweza utu wake.

Mukiza anasema aina hiyo ya udhalilishaji inaweza kuwa na athari kwa mtoto, zikiwamo za kisaikolojia.

“Tukumbuke taarifa mbalimbali tunazozipakia kwenye mitandao ya kijamii zinasambaa kwa kasi na kuwafikia watu wengi na hazifutiki upesi au kuziondoa kwenye simu au kompyuta za watu binafsi,” anasema na kuongeza:

“Hii itapeleka mtoto huyu kutambulika vibaya kwa watoto wenzake na watu wazima, wakiwa shuleni au mazingira ya nyumbani awapo na wenzake, hivyo kupelekea kutengwa na kutotengamana na wenzake. Unyanyapaa huu unaambatana na athari kubwa za kisaikolojia.”

Anasema huweza pia kuathiri uhusiano kati ya mtoto na mzazi wake.

“Iwapo mtoto atakuja kufahamu na kuona video ile, ikaongeza na unyanyapaa anaoweza kukumbana nao kutoka kwa watoto wenzake hii inaweza kuathiri uhusiano kati yake na mzazi wake,” anasema.

Mkurugenzi wa taasisi ya kutetea haki za watoto ya Green Kids and Youth Foundation, Vaileth Mwazembe, anasema wazazi, walezi na wadau wa masuala ya ulinzi wa watoto wanapaswa kuongeza nguvu katika utoaji wa elimu ya matumizi sahihi ya mitandao kwa wazazi, walezi, watoto na vijana ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili na vingine visivyo na maadili mitandaoni.

Katika hilo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Manispaa ya Ubungo, mkoani Dar es Salaam, Zainabu Masilamba anasema vitendo vya wazazi kuweka kwenye mitandao maudhui yasiyofaa yakihusisha watoto ni jambo la kukemewa vikali, kwani ni ukiukaji wa sheria ya mtoto.

Anawakumbusha wazazi kuwa, wanapofanya jambo lolote mbele ya mtoto huchangia kumjenga au kumbomoa.

“Hivyo ni muhimu wazazi kuhakikisha wanatumia mitandao katika mtazamo chanya unaozingatia maadili,” anasema.

Akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Jabiri Bakari, anasema mamlaka kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya mawasiliano na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, wanahusika katika kuhamasisha utekelezaji wa Mkakati wa Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mtandaoni (COP).

Hivyo, TCRA inatoa wito na inaendelea kuhamasisha wazazi na walezi kuepuka vitendo vya kupakia maudhui yasiyofaa mtandaoni yanayowahusisha watoto.

Dk Bakari anasema vitendo hivyo vinavunja Sheria ya Ulinzi wa Mtoto.

“Tunawakumbusha kuwa, mtandao hausahau na ni muhimu kulinda mustakabali wa watoto,” anasema.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Nandera Mhando anasema vitendo vya kuwashirikisha watoto katika maudhui yanayokwenda kinyume cha maadili ya kijamii na kisheria ni uvunjifu wa wajibu wa mlezi.

Anasema vitendo hivyo vinaweza kusababisha mhusika kuchukuliwa hatua za kisheria, ikiwamo kulipa faini isiyozidi Sh5 milioni au kufungwa kifungo kisichopungua miezi sita au vyote kwa pamoja.

Si hivyo pekee anasema mtoto anaweza kuwekwa chini ya uangalizi wa ustawi wa jamii, ikiwamo kufanyiwa uchunguzi na maofisa ustawi iwapo mazingira ya malezi yatabainika kuwa si salama kwa malezi na makuzi ya mtoto husika.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 (RE 2019), kila mzazi au mlezi anao wajibu wa msingi kuhakikisha mtoto analindwa dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kudhuru afya, usalama, utu, ustawi au maendeleo ya mtoto,” anasema na kuongeza:

“Ibara ya 9(1) ya Sheria hii inasisitiza haki ya mtoto kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa aina yoyote, ikiwemo manyanyaso ya kimwili, kihisia, kisaikolojia ikiwemo unyanyasaji na udhalilishaji kupitia mitandao.”

Anatoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanalinda haki za mtoto na kwamba, mitandao ya kijamii iwe nyenzo ya elimu na malezi chanya.

“Badala ya kuwahusisha watoto kwenye mambo yanayokiuka maadili, tunawahimiza wazazi kuwashirikisha kwenye maudhui ya kielimu na kimaadili,” anasema.