Tuzo za Serengeti Awards Kufanyika Disemba 19 jijini Arusha – Global Publishers

KATIBU Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema Tuzo za Uhifadhi na Utalii maarufu kama Serengeti Awards zitafanyika Disemba 19, 2025 jijini Arusha.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 27, 2025 katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani kwenye Kreta ya Ngorongoro, Dkt. Abbasi amesema tuzo hizo zina lengo la kutambua, kuheshimu na kusherehekea mchango wa wadau mbalimbali katika sekta ya uhifadhi na utalii nchini.

Amefafanua kuwa jumla ya tuzo 56 zitatolewa katika makundi saba ambazo ni kura za wananchi kuonesha ni nani anayetambulika zaidi kwa mchango wake katika sekta hiyo, kampuni na waendeshaji wa shughuli za utalii waliobobea katika ubunifu na ubora wa huduma pamoja na waongoza watalii katika taaluma mbalimbali ikiwamo safari, mlima na utamaduni.

Zingine ni tuzo kwa nyumba za kulala wageni na migahawa bora, taasisi, vikundi na watu binafsi wanaoongoza katika juhudi za kuhifadhi maliasili, taasisi na kampuni zinazojitokeza kuonesha vivutio kupitia maonesho ya kitaifa na kimataifa, na washirika, taasisi au watu binafsi waliotoa mchango wa kipekee katika sekta ya uhifadhi na utalii.

Dk. Abbasi amesema dirisha la kupokea maombi ya kushiriki kuwania tuzo hizo litafunguliwa Oktoba 10 hadi 31, 2025 kupitia tovuti rasmi ya wizara: https://serengetiawards.maliasili.go.tz.

“Wadau wote wenye sifa wataweza kushiriki na hafla ya utoaji rasmi wa tuzo itafanyika Desemba 19, 2025 jijini Arusha,” amesema.

Awali, ameeleza kuwa tuzo hizo zilizinduliwa Disemba 20, 2024 jijini Arusha ambapo pia baadhi ya wadau walitunukiwa tuzo za heshima kwa mchango wao katika kukuza uhifadhi na utalii nchini.