JANA Yanga na Singida Black Stars zilikamilisha vibarua vya mechi za marudiano katika michuano ya kimataifa, lakini leo ni zamu ya Simba na Azam.
Timu hizo zinaingia uwanjani zikiwa na mtaji wa ushindi baada ya kufanya vizuri wikiendi iliyopita zikiwa ugenini ambapo pia hazikuruhusu mabao.
Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika inaikaribisha Gaborone United kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 10:00 jioni baada ya ugenini kushinda bao 1-0, kisha saa 11:00 jioni ni Azam dhidi ya Al Merrikh Bentiu mechi ikichezwa Uwanja wa Azam Complex. Azam ilishinda 2-0 huko Sudan Kusini.
SIMBA VS GABORONE
Wekundu wa Msimbazi wanaingia uwanjani wakiwa na kocha mwingine tofauti na yule aliyekiongoza kikosi kushinda ugenini wikiendi iliyopita. Kuondoka kwa Fadlu Davids aliyetimkia Raja Casablanca, Simba imempa nafasi Hemed Suleima ‘Morocco’ kusimamia mechi hii tu, kisha wanafanya mchakato wa kocha mpya ambaye muda wowote kuanzia sasa atatambulishwa.
Mbali na kukosekana Fadlu, pia Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi, hatakuwa sehemu ya benchi la ufundi kwani anatumikia adhabu ya kadi nyekundi.
Elie Mpanzu ndiye aliipa jeuri Simba ugenini Botswana baada ya kufunga bao pekee kwa kichwa dakika ya 16 akiunganisha krosi ya nahodha, Shomari Kapombe.
Katika mechi ya leo, Simba imepata nguvu baada ya kiungo wake mkabaji, Yusuph Kagoma kurejea baada ya adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa msimu uliopita katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane kumalizika.
Simba imekuwa na rekodi bora dhidi ya timu za Botswana lakini pia ina kumbukumbu ya kuzuiwa kusonga mbele 2021 ilipofungwa nyumbani 3-1.
Bila ya mashabiki, Simba inakwenda kuikabili Gaborone United, timu ambayo imekuwa ngumu katika kuruhusu nyavu zake kutikiswa kwani msimu huu kwenye Ligi ya Botswana imeshuka dimbani mara nne na kufungwa mabao mawili pekee.
Jeuri kubwa ya Simba licha ya kucheza bila ya mashabiki, timu hiyo ina rekodi bora ya kutopoteza kwenye mechi 11 mfululizo za CAF ikiwa nyumbani kufuatia kushinda tisa na sare mbili tangu mara ya mwisho ifungwe 0-3 na Raja Casablanca Februari 18, 2023, lakini ikumbuke mwaka 2021 ilishinda ugenini nchini Botswana, ikaja kufungwa nyumbani na kutolewa.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Hemed Suleiman ‘Morocco’ alisema anatarajia mechi ngumu na ya ushindani lakini wapo tayari kuhakikisha timu hiyo inavuka kwenda hatua inayofuata bila ya kuangalia walichovuna ugenini.
Morocco alisema wanafahamu kwamba bado hawapo katika nafasi nzuri na tayari wamefanyia kazi makosa ya mechi ya kwanza ugenini, hivyo wanaamini mechi hiyo itakuwa ni muhimu kwao kufanya vizuri.
“Bao moja ugenini sio la kujiamini sana nyumbani, kama wao waliruhusu na sisi tunaweza kufanya hivyo, kilichopo sasa ni kuhakikisha tutafanya kazi yetu kwa kuipambania timu ifanye vizuri.
“Sijawahi kupoteza kwenye mechi ya kwanza ya mashindano, naamini wachezaji wangu wapo tayari na watapambana kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri na kufuzu hatua inayofuata.
“Sina presha na sijawahi kuwa na presha kwenye mambo ya mpira, tumejiandaa na tunawaahidi mashabiki kuwa tutawapa furaha huko watakapokuwa lakini na wao watuombee,” alisema Morocco.
Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe, alisema kwa upande wao wachezaji wapo tayari na wanatarajia dakika 90 mpya ambazo zinawahitaji kupata ushindi ili kufikia malengo.
“Matarajio yetu msimu huu ni makubwa na ili kufikia hatua hiyo ni lazima kupata matokeo mazuri kwenye mechi za awali, tupo tayari kuhakikisha tunapambana na kupata ushindi.
“Matokeo yaliyopita tumeyasahau, tunaingia kupambania dakika 90 bora na za ushindi, kwetu matarajio ni kucheza mechi ngumu kwani hata wapinzani wetu wamekuja kutafuta matokeo lakini kitu tulichokiandaa tutakifanyia kazi Uwanja wa Mkapa,” alisema Kapombe.
Kocha wa Gaborone United, Khalid Niyonzima, alisema hawana presha yoyote kuelelea mechi ya leo dhidi ya Simba huku akiwahakikishia furaha mashabiki wa timu hiyo.
Alisema wapo tayari kuibuka na ushindi ugenini na kutinga hatua inayofuata huku akiweka wazi kwamba wataingia kwenye mechi hiyo wakiwa hawana cha kupoteza.
Aliongeza kwamba, wanaifahamu Simba na wana matarajio makubwa kupata matokeo mazuri, huku akijivunia kikosi chake ambacho amekitaja kuwa kipo tayari kutoa burudani kikiwa hakina presha kutokana na kucheza bila ya mashabiki.
“Bao moja halifanyi kuwa chini tukiamini tumepoteza, kama wao walipata ushindi kwetu na sisi tutapata kwao, tunakutana na timu ambayo tunaifahamu, hatuna presha, tupo tayari kushindana.
“Wachezaji wanafahamu wanakutana na Simba ambayo imewafunga nyumbani na wao wamekuja kutafuta matokeo, hawatarajii mchezo rahisi, lakini mashabiki wa Gaborone watarajie furaha baada ya mchezo,” alisema Niyonzima.
AZAM VS AL MERREIKH BENTIU
Azam imekuwa na mwanzo mzuri msimu huu kwani licha ya kushinda mechi ya kwanza ya kimataifa dhidi ya Al Merreikh Bentiu ugenini nchini Sudan Kusini kwa mabao 2-0, pia ikaipa Mbeya City kichapo kama hicho kwenye Ligi Kuu Bara.
Hiyo inaonyesha ni mwanzo mzuri wa Kocha Florent Ibenge ambaye huu ni msimu wake wa kwanza kufundisha timu ya Tanzania huku mashabiki wengi wa Azam wakiwa na matarajio makubwa ya timu hiyo kufuzu kwa mara ya kwanza hatua ya makundi.
Rekodi zinaonesha mara zote Azam iliposhiriki mashindano ya CAF, haijawahi kucheza hatua ya makundi ambapo sasa Ibenge ana kazi ya kufanya na kikosi hicho.
Azam inaona kuna mwanga wa kucheza makundi kwani ikifanikiwa kuiondoa Al Merrikh Bentiu, itacheza dhidi ya KMKM ya Zanzibar.