Mbeya. Mgombea urais wa Chama cha Makini, Coaster Kibonde, ametumia asili yake ya kuzaliwa na kulelewa katika mji mdogo wa Mbalizi, Wilaya ya Mbeya, kuwaomba wananchi wa eneo hilo, huku akiahidi matrekta kwa wakulima na mshahara wa kima cha chini wa Sh600,000 endapo atapewa ridhaa ya kuunda Serikali.
Akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika jana Septemba 27, 2025, katika viwanja vya Tarafani, Mbalizi, Kibonde amesema kuzaliwa kwake katika mji huo ni fursa ya kipekee kwa wakazi wa eneo hilo kumuunga mkono kwa uzalendo.
Kibonde amesema sera za chama chake zinajikita katika kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta za kilimo, elimu na afya.
Ameahidi kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali hadi chuo kikuu bila michango, sambamba na kuhakikisha elimu hiyo inalenga ujuzi utakaowawezesha wahitimu kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi.
“Serikali ya Makini itatoa elimu yenye stadi za kazi na tutasomesha wanafunzi hata nje ya nchi,” amesema.
Katika sekta ya kilimo, ameahidi vijana watapatiwa ekari tano kila mmoja zenye hati miliki ili kuondoa changamoto ya kukosa mikopo kutokana na kutokuwa na dhamana.
Pia amesema hakutakuwa na kilimo cha jembe la mkono kwa sababu wakulima watapatiwa matrekta na serikali itaunda soko huria litakalowawezesha kuuza mazao yao popote wanapopenda.
Kwa upande wa afya, Kibonde ameahidi kujenga hospitali za kata zilizo na vifaa tiba na wataalamu wa kutosha, huku akisisitiza kuwa serikali yake haitamvumilia mtoa huduma atakayesababisha kifo kwa uzembe.

Mgombea huyo akigawa kadi za chama hicho kwa baadhi ya wananchi wa mji huo.
“Falsafa yangu ni kuwatumikia wananchi, naomba kura zenu Oktoba 29, ili niunganishe wilaya kwa wilaya kwa kiwango cha lami,” amesema.
Ameongeza kuwa serikali yake itatoa mikopo isiyo na riba kwa wafanyabiashara wadogo (machinga) na kwamba kima cha chini cha mshahara kitaongezwa hadi kufikia Sh600,000.
Kwa upande wake, mgombea mwenza wa chama hicho, Azza Haji Suleiman, amesema chama cha Makini kimezunguka maeneo mbalimbali ya Mbeya na kujionea changamoto zinazowakabili wananchi.
Hivyo, ameahidi kipaumbele cha kwanza kwa chama chao, kikifanikiwa kuingia madarakani, ni sekta ya afya kwa kuanzisha huduma mpya itakayojulikana kama ‘Makini Care’ itakayotolewa bure.
“Afya ni msingi wa mipango mingine yote. Tukiwa na wananchi wenye afya bora, kila jambo linawezekana,” amesema.
Aidha, amewataka wananchi kuepuka kurubuniwa kwa fedha na kusisitiza kuwa kura ni chombo cha msingi cha kulinda amani na hatima ya maisha yao.
Makamu Mwenyekiti wa chama hicho na mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo, Mkoa wa Dar es Salaam, Grace Ngonyani, amewahimiza wakazi wa Mbalizi kumpigia kura Kibonde akisema ni fursa ya kipekee kumchagua mgombea mzaliwa wa eneo hilo.
“Chama cha Makini kina sera bora katika elimu, afya na kilimo. Tunawaomba kura kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais,” amesema Ngonyani.
Awali, Naibu Katibu Mwenezi wa chama hicho, Ramadan Bambo, amewataka wananchi kuachana na mtazamo wa kupiga kura kwa mazoea na badala yake watoe nafasi kwa chama kipya chenye dhamira ya kufanya mabadiliko.
Amebainisha kuwa tafiti za chama hicho zimeonesha uwepo wa ardhi kubwa inayomilikiwa na viongozi wachache, na kwamba serikali ya Makini itagawa ardhi hiyo kwa vijana.
“Niwaombe Oktoba 29 msifanye makosa. Mpeni kura Kibonde ili aongoze nchi kwa maendeleo. Sisi hatutoleta ushawishi wa pesa wala kusomba watu mikutanoni,” amesema.