Riadha inalipa…Simbu ajazwa mamilioni, nyumba

WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amemkabidhi mwanariadha Alphonce Simbu hundi ya Sh20 milioni kwa kuitangaza vyema Tanzania baada ya kushinda medali ya dhahabu katika michuano ya Mbio za Riadha za Dunia zilizofanyika hivi karibuni, jijini Tokyo Japan huku akiahidiwa kupewa nyumba na Rais Samia Suluhu Hassan.

Fedha hizo zilizotolewa na serikali kama ‘asante’ kwa Simbu kutoka na ushindi huo alioupata katika mbio hizo za dunia ambazo zilimwezesha pia kuvuna dola 70,000 (zaidi ya Sh170 milioni) mbali na kupandishwa cheo jeshini kutoka sajenti hadi kuwa sajentitaji.

Waziri Mkuu alisema juzi katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaamu kuwa, serikali imeamua kumzawadia Simbu kwa sababu ameinyanyua juu sana hadhi ya Tanzania kimataifa na kuifanya nchi kuzidi kujulikana kimataifa kama gwiji wa mbio za ndefu za Marathon.

Katika hafla hiyo ya kuwapongeza wanamichezo waliofanya vyema mbali na Simbu pia klabyu ya JKT Queens, wachezaji wa Kriketi, Futsal nao walizawadiwa hundi ya Sh 10 milioni kila moja.

SIMB 01


SIMB 01

Waziri Mkuu alitoa pongezi hizo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla hiyo, ambapo Majaliwa alitangaza pia kuwa Rais amempatia Simbu zawadi ya nyumba jijini Dodoma.

“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia ameandaa nyumba iliyopo mkoani Dodoma, ambayo itakabidhiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na zoezi hilo lisichukue muda mrefu kuanzia leo (juzi Jumamosi), tusiwe tunatamka ahadi za viongozi halafu zinakaa muda ambao mtu anajiuliza,” alisema Waziri Mkuu.

Majaliwa alisema, Simbu ameandika ukurasa wa upekee kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa tuzo ya dhahabu katika Marathoni ya Dunia ya mwaka 2025.

SIM 02


“Haya ni mashindano makubwa zaidi ya riadha duniani baada ya Michezo ya Olimpiki, yakihusisha wanariadha bora kutoka mataifa yote duniani,” alisema Waziri Mkuu na kuongeza; “Matokeo tunayoyashuhudia hivi sasa ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ikiwamo ukarabati wa viwanja na kuongezwa kwa bajeti kutoka Shilingi 38 bilioni mwaka 2022 hadi bilioni 326 mwaka 2025/2026.”