Vohra, Karan waitwa Guru Nanak Rally

CHAMA kinachosimamia mchezo wa mbio za magari nchini (AAT) kimemtangaza dereva Ahmed Huwel kuwa kinara wa msimamo wa mbio za kusaka taji la taifa kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa msimamo wa AAT, Huwel, ambaye ameingia na gari isiyokamatika ya Toyota Yaris, anaongoza akiwa na pointi 105 na kumuacha mpinzani wake wa karibu, Randeep Singh wa pointi 17.

Matokeo haya yanauweka mkoa wa Iringa karibu kabisa na taji la ubingwa wa mbio za magari kwa mwaka huu, hali ambayo inatishia himaya ya Manveer Birdi wa Dar es Salaam ambaye ndiye bingwa mtetezi.

Jawabu la kama Mkoa wa Iringa utaweza kuuvua taji Mkoa wa Dar es Salaam litapatikana mwezi ujao mkoani Arusha ambako mbio za Guru Nanak zitachezwa ili kutamatisha kalenda ya mbio za magari kwa mwaka huu.

GUR 01


Ili kunogesha zaidi upinzani katika raundi hii ya tano na ya mwisho kwa mwaka huu, madereva na wadau wa mchezo wa mbio za magari nchini wameanza mchakato wa kuwaalika madereva hodari wa Kenya, Samman Vohra na Karan Patel, ambao walitamba sana katika mashindano ya mbio za magari ubingwa wa Afrika.

Wadau wa mbio za magari wanaamini kuwaleta Arusha mabingwa hawa kutoka Kenya kutasaidia kuongeza ushindani na kuzipa mbio zao Guru Nanak msisimko mkubwa na pia taswira ya kimataifa.

Kwa maandalizi ya raundi ya hitimisho, Huwel ameweza kujikusanyia jumla ya pointi 105 akianza na pointi 35 (30+5) baada ya kushinda Mkwawa Rally mwezi Agosti kabla ya kutwaa pointi 70 (60+10) kwa kushinda Mkwawa Rally of Tanzania mwishoni mwa juma.

GUR 02


Randeep Singh ni wa pili akiwa na jumla ya pointi 88. Alianza na pointi 35 (30+5) kwa kushinda raundi ya pili mkoani Dar es Salaam, aliongeza pointi 15(11+4) katika raundi ya tatu kabla ya kutwaa pointi 38 (30+8) katika mbio za Mkwawa Rally of Tanzania.

Nafasi ya tatu inashikiliwa na Waleed Nahdi wa Morogoro mwenye pointi 80 wakati nafasi ya nne inashikiliwa pia na dereva kutoka Morogoro, Samir Shanto mwenye pointi 74.

Dereva kutoka Arusha, Gurpal Sandhu ni wa tano akibeba bango la pointi 73 mbele ya bingwa mtetezi Manveer Birdi katika nafasi ya sita akitwaa jumla ya pointi 62.

Dereva kutoka Dar es Salaam, Shehzad Munge anashika nafasi ya saba akiwa na pointi 62 akimuacha Prince Charles Nyerere wa Arusha mwenye pointi 40, kwa pointi 22.