MAKOCHA 10 kati ya 30 wamefaulu kozi ya ukocha wa Taekwondo inayotambuliwa na Shirikisho la mchezo huo la Dunia.
Kozi hiyo iliyofanyika kwenye kituo cha Olympafrica kilichopo Kibaha, Pwani iliendeshwa na mkufunzi kutoka Shirikisho la Taekwondo la Dunia, Dk Jun Cheol Yoon.
Yoon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Waamuzi wa mchezo huo duniani amesema ambacho amekiona kwa makocha hao ni ufundi na mbinu kuongezeka kila siku ya mafunzo.
“Kufaulu au kufeli kunategemea, lakini makocha wote walijitahidi na kila mmoja alipambana kila alivyoweza, tangu siku ya kwanza niliwaeleza ugumu wa mafunzo haya. Hivi sasa kila mmoja wa wahitimu yupo kwenye maumivu, lakini ni maumivu yenye tija, mlivyokuja si mnavyoondoka, mbinu na ufundi vimeongezeka kwa kila mmoja wenu,” alisema Dk Yoon.
Dk Yoon alisema wiki ya kwanza ya mafunzo alibaini kila mmoja ana kitu spesho cha kumuendeleza katika mchezo wa Taekwondo.

Katika makocha hao, 10 ndio wamefaulu kwa ngazi ya awali ya mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) na kudhaminiwa na Kituo cha Misaada cha Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) cha Olympic Solidarity (OS) na kuratibiwa na Shirikisho la Taekwondo Tanzania (TTF).
Rais wa TTF, Ramoudh Ally akizungumzia ufaulu huo, amesema unakwenda kuongeza chachu ya kuenea kwa mchezo huo nchini.
“Makocha 10 waliofaulu, kila mmoja akifungua klabu ya taekwondo katika eneo lake na kuwa na wachezaji 30 kila mmoja, tutakuwa na wachezaji wapya 300, huu utakuwa mwanzo mzuri kwa mchezo wetu,” alisema Ally na kuwaambia makocha hao kama watahitaji vitendea kazi basi wawasiliane na Shirikisho kwa msaada zaidi.
Ally amesema kupitia mafunzo hayo, wanahitaji kutengeneza Taekwondo ya kizazi kijacho ambacho kitafuzu kushiriki Olimpiki ya 2032, wakiweka mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Alisema pia kwa wale ambao alama za ufaulu hazijatosha, Shirikisho litafanya utaratibu ili kupata kozi nyingine za kimataifa kupitia Shirikisho la mchezo huo la kimataifa ili wasome tena.
“Tutatoa taarifa, lengo ni kuwa na idadi kubwa ya makocha wenye sifa,” alisema na kuongeza kuwa, kwa wale waliofaulu Shirikisho litawapa leseni za ukocha wakati huo huo wakisubiri leseni kama hizo kutoka Shirikisho la Taekwondo la Dunia.
Akifunga mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa TOC, Henry Tandau amewataka makocha waliohitimu kutumia elimu waliyoipata kwa maslahi ya mchezo huo nchini.
“Tunapaswa tujiulize Taekwondo itakuwa wapi kwa miaka 10 ijayo? Kama mtakuwa na lengo na kulifanyia kazi, mfano mkakati wa kushiriki Olimpiki 2032 mnaweza,” alisema Tandau.
Alisema ufaulu wa makocha 10 pekee hautoshelezi akibainisha hata waliofaulu hawapaswi kuishia levo hiyo, wajiendeleze ili wafike mbali zaidi.
“Lazima muwe na wivu wa maendeleo, huwa nikienda kwenye mashindano makubwa, siwaoni makocha au marefa wengi wa Tanzania lazima tujipange, kwani bila mipango hauendi popote,” alisema.

Akizungumzia ushiriki wao, mmoja wa wahitimu kutoka Dar es Salaam, Janeth Oscar alisema programu waliyopewa na Grandmaster Yoon akishirikiana na Master David Samson imewajenga.
“Tunakwenda kuifanyia kazi taaluma tuliyoipata, japo mchezo wa taekwondo bado una changamoto ya uhaba wa vifaa mazoezi na uhaba wa ukumbi wa kisasa wa kufanyia mazoezi,” alisema.
Katika mafunzo hayo, Rashid Yahaya Rashid alitajwa na Dk Yoon kama kocha aliyeonyesha kiwango kizuri wakati wa mafunzo.