Dar es Salaam. Vinyozi, wasusi, wabunifu wa michoro, wapigapicha, wachoraji na wataalamu wengine wa kazi za ubunifu sasa watalazimika kusajiliwa na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) ili kuendesha shughuli zao kihalali nchini Tanzania.
Agizo hili jipya linatokana na marekebisho ya kanuni za Basata zilizochapishwa katika Gazeti la Serikali Juni 30, 2025, na kuashiria mabadiliko makubwa katika sekta ya ubunifu nchini kwa kutambua rasmi sekta ambazo zimekuwa zikifanya kazi bila kudhibitiwa rasmi kwa muda mrefu.
Marekebisho hayo pia yamepunguza gharama za usajili, ambapo ada ya kujiunga imepunguzwa kutoka Sh40,000 hadi Sh20,000 na ada ya uhuishaji kila mwaka ni Sh10,000.
Kwa mujibu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Basata, mabadiliko hayo yameletwa ili kuwasogeza wasanii karibu zaidi na mifumo ya msaada ya Serikali.
“Lengo letu si kuua ndoto zao, bali kuwasogeza karibu na Serikali ili waweze kupata fursa kama ufadhili kutoka kwenye Mfuko wa Taifa wa Sanaa,” limeeleza baraza hilo.
Basata imeeleza kuwa mamlaka yake sasa inahusisha makundi matatu makuu ambayo ni muziki, sanaa za maonyesho na sanaa za ubunifu.
Sanaa za maonyesho zinajumuisha ngoma za asili, sarakasi na maonesho ya uchawi, huku sanaa za ubunifu zikihusisha taaluma kama ususi wa nywele, vinyozi, upigaji picha, ubunifu wa michoro na uchoraji.
Baraza limesisitiza kuwa hata huduma za saluni zinahusishwa katika kundi hilo kwa kuzitambua kama aina ya ubunifu wa mitindo.
“Leo hii ukienda saluni ukapewa mtindo mpya wa nywele, kinyozi ametumia ubunifu. Au ukiwa na kipara na wakaweka nywele bandia, hiyo pia ni kazi ya ubunifu,” wameeleza Basata.
Maofisa wa Basata wamesema kuwa kuhalalisha sekta hiuo kutasaidia si tu kuitambua rasmi, bali pia kuimarisha mchango wake katika uchumi kupitia uundaji wa ajira.
“Wasanii wengi waliofanikiwa wameweza kuajiri watu wengine, ambapo utakuta msanii mmoja ana wakili, mhasibu na watu wengine wanaosimamia kazi zake. Ikiwa watu wote hao wanategemea msanii mmoja, maana yake ajira zimetengenezwa,” limeongeza baraza hilo
Kwa kuingiza makundi mapya, Basata inatarajia kujenga uchumi endelevu wa ubunifu.
“Kupitia mageuzi haya, tumeweza kuwarejesha wasanii waliokuwa hawajihusishi tena ili nao wajikwamue. Hii ni sehemu ya kuhakikisha sekta hizi zinaheshimiwa kama ilivyo muziki na sanaa nyingine,” wameeleza.
Basata pia imefafanua kuwa vyombo vya habari vinatarajiwa kujisajili na baraza iwapo vitahusika na uandaaji wa matukio ya kisanii.
“Utakuta kuna kampuni za vyombo vya habari zinaendesha matamasha na maonyesho. Ikiwa matukio hayo yanaangukia kwenye makundi ya Basata, basi lazima wazingatie kanuni. Sisi tunashughulika na sekta zote za sanaa isipokuwa filamu,” wameeleza.
Katika baadhi ya matukio, waandishi wa habari wanaofanya kazi pia kama mapromota au mameneja wa wasanii wanaweza kuhitajika kuwa na leseni kutoka Basata.
Baraza limekiri kufahamu malalamiko kutoka kwa wamiliki wa saluni ambao biashara zao zimefungwa, lakini wameeleza kuwa kufungwa huko kunatokana na ushirikiano kati ya Basata na taasisi nyingine kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela).
“Ukimuona mtu anakumbwa na hali kama hiyo, ni kwa sababu mamlaka husika zinachukua hatua, hasa pale mtu anapokuwa hajakamilisha vibali muhimu,” wameeleza Basata.
Kwa wataalamu, mabadiliko hayo yanaweza kuleta fursa pamoja na changamoto.
Avila Chaula, anayejulikana zaidi kama Allie Stylist, mwanachama wa Chama cha Wasusi Tanzania, amesema mageuzi hayo ni hatua ya maendeleo japokuwa uelewa bado ni mdogo.
“Ususi sasa uko rasmi chini ya usimamizi wa Basata, na wamekuwa kama washauri kwetu. Hata hivyo, wasusi wengi bado hawajafahamu kuhusu mahitaji haya,” amesema.
Chaula amesisitiza kuwa usajili unahitajika kwa msusi mmoja mmoja, si kwa wamiliki wa saluni pekee.
“Nikimiliki saluni yenye wasusi kadhaa, kila msusi bado anatakiwa kujisajili binafsi,” amefafanua na kuongeza kuwa usajili unafungua pia milango ya kimataifa.
“Ukisajiliwa, ni rahisi zaidi kupata visa na vibali vya kazi nje ya nchi. Nikitaka kusafiri kwenda China au Marekani kufanya kazi, kutambuliwa rasmi na Basata hurahisisha mchakato,” ameeleza Chaula.
Hata hivyo, amehimiza Basata pamoja na sekta husika kuongeza juhudi za uelimishaji.
“Maofisa wa biashara sasa wanaomba vyeti vya Basata, na hata Brela wanawaelekeza waombaji kwanza waende Basata. Hii inaonesha jinsi ilivyo muhimu kwa wasusi kujisajili. Basata waendelee kutuelimisha, lakini pia wasusi tujitokeze na tushirikiane zaidi,” amesema.
Kwa upande mwingine, vinyozi wamekiri kuwa hatua hii ni mpya kwao, lakini wako tayari kuitii iwapo gharama zitakuwa nafuu.
“Binafsi nimekuwa kinyozi kwa miaka mingi sasa na sijawahi kukutana na hitaji kama hili, lakini kama Serikali imeweka mfumo mzuri wa kututambua na kutuwezesha kupata mikopo, basi naona ni jambo jema litakalotusaidia tunapopitia changamoto,” amesema Dulla Hamadi, kinyozi kutoka Sinza, Dar es Salaam.
Msusi Habiba Mohammed wa Kijitonyama naye amekubali mageuzi hayo kwa masharti kuwa mikopo itapatikana kwa urahisi.
“Zaidi ya masuala haya ya usajili, iwapo baraza linanitambua na ninaweza kupata mkopo, hilo litakuwa jambo chanya na itaonyesha araza limepiga hatua ya kweli,” amesema.
Kwa sasa, mafanikio ya mageuzi haya yanategemea kasi ya Basata na wadau wake katika kusambaza uelewa kwa sekta ya ubunifu ambayo ni pana na isiyo rasmi kwa kiasi kikubwa.