Mwili wa Askofu Rugambwa wapokelewa Bukoba

Bukoba. Mwili wa Askofu Rugambwa, aliyekuwa Balozi wa Papa nchini New Zealand, umepokelewa na mamia ya waumini wa Kanisa Katoliki mkoani Kagera, uwanja wa ndege wa Bukoba ukiwasili kutoka Dar es Salaam.

Mwili huo umewasili saa 6:17 mchana kwa ndege ya kampuni ya Air Tanzania.

Baada ya kupokelewa uwanja wa ndege, umepelekwa makao makuu ya Kanisa Kuu Katoliki Bukoba (Cathedral) huku ukisindikizwa na viongozi wakuu wa kanisa, viongozi wa Serikali pamoja na waumini.

Ibada mbili za kuupokea mwili huo zimeendeshwa; moja ikifanyika uwanja wa ndege na nyingine katika Kanisa Kuu la Bikira Maria Mama Mwenye Huruma (Cathedral Bukoba) kwa ajili ya taratibu za mazishi kesho, Septemba 29, 2025. Ibada hizo zimeongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Bukoba, Jovitus Mwijage.

Aidha, katika mapokezi ya mwili huo, walikuwepo viongozi wengine kama Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu Desderius Rwoma, Askofu msaidizi mstaafu wa Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu Methodius Kilaini.

Picha ya waumini na  Gari lilobeba Jeneza la mwili wa Askofu Novatus Rugambwa kuelekea kanisa kuu Katoliki Bukoba.



Wengine ni Askofu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Thaddaeus Ruwa’ichi; Askofu msaidizi wa Dar es Salaam, Mhashamu Henry Mchamungu; Askofu wa Jimbo Katoliki Moshi, Mhashamu Ludivick Minde; na Askofu wa Jimbo Katoliki Mbinga, Mhashamu Chrizostom Ndimbo.

Katika msafara wa mapokezi ya mwili wa Askofu Rugambwa, alikuwepo pia Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima, aliyeongozana na baadhi ya watumishi wa ofisi yake.

Baada ya ibada ya pili, Askofu Mwijage, amewaeleza waumini wa kanisa hilo kuwa leo itafanyika ibada ya kuombea mwili wa marehemu majira ya jioni, itakayojumuisha waumini wote na wananchi waliokuja kusindikiza mwili wa Askofu Rugambwa.