SINGIDA Black Stars imetinga raundi ya pili ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuing’oa Rayon Sports ya Rwanda kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1, huku kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi akisema anajipanga upya ili kuhakikisha wanafuzu hatua ya makundi.
Gamondi mwenye rekodi ya kuifikisha Yanga katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili mfululizo wakati akiinoa, alisema anajua mechi ijayo ya raundi ya pili ni ngumu, lakini atajipanga na jeshi alilonalo ili kuona Singida inaendelea kufanya vizuri kimataifa.
Singida jana usiku ilipata ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, ilipokuwa ikirudiana na Rayon ambao ilikubali kichapo cha 1-0 jijini Kigali wiki iliyopita na sasa inajiandaa kukutana na mshindi wa mechi kati ya Flambeau du Centre ya Burundi na Al Akhdar ya Libya. Timu hizo mbili zilikuwa zikirudiana jana Jumapili, huku Warundi wakiwa na faida ya ushindi wa 2-1 iliyopata wiki iliyopita.

“Tunashukuru tumefuzu hatua inayofuata, hii ilikuwa mechi ngumu na yenye ushindani, lakini bahati imekuwa kwetu kwa kushinda tena. Tuna kazi kubwa ya kujipanga kwa mechi ijayo, ili kutimiza lengo la kuona tunafika mbali katika michuano hii,” alisema Gamondi aliyeandika rekodi kadhaa za kusisimua akiwa Yanga ikiwemo kuifikisha makundi ya Ligi ya Mabingwa baada ya kupita miaka 25.
Pia aliweka rekodi ya kuifunga na kuing’oa Al Merrikh ya Sudan katika michuano ya kimataifa, mbali na kuiongoza Yanga mechi nane za kwanza za msimu uliopita wa Ligi Kuu kwa kushinda zote na kutoruhusu bao lolote kabla ya kutibuliwa na Azam iliyoinfunga 1-0 na kugongwa tena na Tabora United (sasa TRA United) kwa mabao 3-1 nyumbani na kusababisha kutimuliwa Jangwani.
Katika mechi ya jana, Rayon ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Glouire Tambwe dakika ya 38 kabla ya Idriss Diomande kuisawazishia Singida kwa pasi na Elvis Rupia dakika ya 44 na beki wa kati Anthony Tra BI kufunga bao la ushindi lililoihakikishia timu hiyo kusonga mbele.

Singida inasaka rekodi iliyowahi kuwekwa na Namungo ilipotinga makundi msimu wa 2020-2021 ikiwa ni timu nje ya Simba ya Yanga, japo ilishindwa kupata ushindi wala kufunga bao lolote katika kundi ililopangwa pamoja na Nkana ya Zambia, Pyramids ya Misri na Raja Casablanca ya Morocco.
Singida BS imeungana na KMKM na Yanga zilizotangulia mapema kutinga raundi ya pili ya michuano ya CAF ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Mlandege ikiaga licha ya kushinda jana mabao 3-2 mbele ya Insurance ya Ethiopia baada ya awali kulala ugenini mabao 2-0, huku Simba na Azam zilikuwa uwanjani jana kumalizana na Gaborone United na Al Merreikh Bentiu.
Ratiba inaonyesha mechi ya raundi ya pili ya michuano ya CAF imepangwa kupigwa kati ya Oktoba 17-19 na zile za marudiano ni Oktoba 24-26, huku kwa Kombe la Shirikisho mechi zipo ifuatavyo katika jedwali.