Kinda Azam bado kidogo England

KINDA la Azam FC, Abdulkarim Kiswanya amesema amemaliza wiki moja ya kufanya majaribio kwenye klabu ya QPR inayoshiriki Championship, England.

Kiungo huyo aliongozana na Makamu wa Rais wa Azam, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alipomsindikiza kuhakikisha mambo yanakuwa sawa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kiswanya alisema tayari amemaliza majaribio na anarejea nchini leo huku akisubiri majibu kama amefaulu ama la.

Aliongeza hadi sasa kuna mazungumzo yanaendelea baina ya QPR na uongozi wa Azam na bado hajafahamu kama dili hilo litakamilika au la.

“Leo tunarejea nchini na nilikuwa England kwa wiki nzima. Sijajua kinachoendelea kwa sasa, lakini nafahamu kuna mazungumzo baina ya Azam na QPR, kwa hiyo mambo yakiwa sawa yatawekwa wazi,” alisema Kiswanya na kuongeza:

“Ni ndoto ya kila mchezaji kucheza ligi kubwa. Naamini kama nitapata nafasi, itakuwa moja ya ndoto yangu imetimia  kucheza nje ya Tanzania na mimi nipate uzoefu. Hapa nilipo ni sehemu sahihi kwa sababu Azam imetoa na kukuza wachezaji wengi kimataifa.”

Kama Kiswanya atafanikiwa kusajiliwa na timu hiyo, atakuwa Mtanzania wa pili kucheza huko baada ya Kealey Adamson kuingia dirisha hili la kiangazi.

Msimu uliopita QPR ilimaliza nafasi ya 15 ikiwa na pointi 56 kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 25.

Msimu huu tayari ipo nafasi ya tisa baada ya kucheza mechi sita na kukusanya pointi 10.