Njombe. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu ameahidi kufufua viwanda viwili vya chai vilivyofungwa katika eneo la Lupembe mkoani Njombe.
Amesema chama hicho kitafanya hivyo ndani ya siku 100 endapo kitapatiwa ridhaa na wananchi Oktoba 29, 2025.
Mwalimu amesema serikali yake haiwezi kuridhia eneo kama la Njombe linalozalisha zao la chai kwa wingi likose viwanda vya kutosha kuchakata zao hilo ili kuongeza thamani, kuingiza fedha za kigeni na kuongeza ajira kwa vijana wa Kitanzania.
Akiwahubia wakazi wa Lupembe leo Jumapili, Septemba 28, 2025 katika mwendelezo wa kampeni zake, Mwalimu amesema kufungwa kwa viwanda hivyo kikiwamo cha Mgombola, ni sehemu ya mkakati wa kuwaweka wananchi katika umasikini ili waendelee kuwa tegemezi kwa wanasiasa.
“Nawaahidi watu wa Lupembe, nipeni siku 100. Viwanda vya chai vilivyofungwa vitafufuliwa. Dunia inahitaji chai, wasiwaambie vingine. Viwanda hivi vimefungwa kwa sababu shida zenu ni mtaji wao,” amesema Mwalimu na kuongeza:
“Wanafanya muwe maskini ili mnapowahitaji muwapigie magoti. Wanajua viwanda vikifanya kazi mtakuwa wajanja, watawala watashindwa kuwabana.”
Mwalimu ameahidi kuwa endapo hakutapatikana mwekezaji mwenye nia njema, basi Serikali itavichukua viwanda hivyo na kuviendesha yenyewe ili kurudisha ajira kwa vijana.
Akiendelea kueleza madhara ya ubinafsishaji usio na tija, Mwalimu ametoa mfano wa viwanda vya chai kuuzwa kwa wawekezaji wa Kenya, ambao ni washindani wakuu wa zao hilo, hali inayodhoofisha ushindani wa Tanzania kimataifa.
“Wameuza viwanda kwa Wakenya, halafu vinakufa makusudi ili vyao vinufaike. Kenya hadi leo hujasikia viwanda vyao vya chai vikifungwa,” ameeleza.
Pia, ametaja makosa yaliyofanywa na Serikali ya CCM kwenye viwanda vya nguo aina ya kanga, vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji wa India walioviuwa, na sasa Tanzania inaongoza kuagiza kanga kutoka nje.
Kando na suala la viwanda, Mwalimu ameahidi kujenga barabara ya lami ya kilomita 65 kutoka Njombe Mjini hadi Lupembe ndani ya miaka mitano ya utawala wake, ili kupunguza gharama za uzalishaji na kurahisisha usafirishaji wa mazao.
“Haiwezekani utajiri wote huu mnashindwa kuletewa barabara bora. Tutaandika historia ya kuwa na lami Lupembe tangu tupate uhuru,” ameahidi.
Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Lupembe kupitia Chaumma, Mgani Hildebrand, ameahidi kuwaletea wananchi maendeleo makubwa endapo atachaguliwa kuwa Mbunge.
Ametaja kipaumbele chake kuwa ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Njombe hadi Madete, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na umeme wa uhakika.
Hildebrand amesema mafanikio ya kweli yanahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya viongozi na wananchi.
“Ninaomba tushirikiane, hakuna kiongozi anayefanikiwa mwenyewe. Tunazo changamoto nyingi, ikiwemo matatizo ya viwanda vya chai. Chai yetu inauzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na wenzetu Wakenya,” amesema.
Amegusia umuhimu wa mikopo kwa wananchi ili waweze kukuza mitaji yao na kufanya shughuli za kiuchumi kwa mafanikio.
Amesema endapo atachaguliwa, ataishi jimboni ili kusikiliza na kushughulikia kero za wananchi kwa karibu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa Chaumma, John Mrema amesema chama hicho kikiingia madarakani kitaweka mazingira bora ya maisha kwa wananchi, ikiwemo kupunguza kodi ya vifaa vya ujenzi ili kuwezesha wananchi kujenga nyumba bora.
“Wachagueni wawakilishi wa Chaumma, ili waingie kwenye vyombo vya maamuzi na kusimamia masuala haya kwa niaba yenu,” amesema Mrema.