Moshi. Wazazi wametakiwa kuwalea watoto katika misingi ya maadili na hofu ya Mungu, ili kujenga jamii yenye kizazi chenye nidhamu na maadili, hatua itakayowezesha kuepuka mmomonyoko wa maadili ambao umeendelea kuwa changamoto kwa Taifa.
Rai hiyo imetolewa leo Septemba 28, 2025 na mwanafunzi wa uchungaji, Neema Mangale wakati akihubiri katika ibada ya sikukuu ya watoto katika Usharika wa Moshi Pasua, Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mangale ameema ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha anamlea mtoto katika njia bora na zenye kumpa mwongozo wa maisha, kwa kuwa mtoto anayekuzwa katika hofu ya Mungu ana nafasi kubwa ya kuwa raia mwema mwenye manufaa kwa Taifa.
Aidha, ameonya wazazi kuepuka vitendo vya kikatili dhidi ya watoto ikiwemo kuwaadhibu kwa kipigo kisichostahili, akisema vitendo hivyo havimsaidii mtoto, bali vinajenga usugu na kumfanya awe na hasira za ndani pamoja na roho ya ukatili.
“Wazazi tuwe karibu na watoto wetu, tuwafundishe maadili na tuwalee katika kumjua Mungu. Tusiruhusu hasira au misukumo ya maisha kutufanya tuwe kikwazo kwa watoto wetu,” amesema.
Amesisitiza kuwa malezi hayapaswi kuachwa mikononi mwa wasaidizi wa nyumbani pekee kwa kisingizio cha wazazi kuwa na shughuli nyingi za kutafuta kipato, badala yake wazazi wanapaswa kutenga muda wa kukaa nao kubaini changamoto wanazokabiliana nazo.
Akizungumzia changamoto za malezi ya sasa, Mangale amesema dunia ya leo inakabiliwa na changamoto kubwa zinazohitaji umakini wa wazazi.
Ametolea mfano ongezeko la maovu katika jamii kama vile ukatili, mauaji na matumizi mabaya ya teknolojia kwa.
“Tujifunze kusikiliza na kukaa karibu na watoto ili kuelewa changamoto wanazopitia nyumbani, shuleni na hata wakiwa mitaani. Jamii inapaswa kushirikiana kukemea maovu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho,” amesema.
Kwa upande wake, Mwinjilisti Lucy Kitema amewataka wazazi kurudi kwenye nafasi zao za malezi, akibainisha kuwa watoto wanaolelewa katika misingi ya kumjua Mungu, huishi kwa hofu ya Mungu na hukwepa vitendo viovu vinavyoweza kuharibu maisha yao.
“Watoto wakilelewa kwenye misingi ya kiroho watakuwa na hofu ya Mungu na wataweza kukimbia uovu. Niombe wazazi turudi kwenye nafasi zetu za malezi na tuhakikishe tunawafuatilia watoto wetu kila hatua wanayokuwepo,” amesema Kitema.
Katika ibada hiyo, baadhi ya watoto wamepata nafasi ya kueleza changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo vitendo vya ukatili, kudharauliwa na hata kutopata muda wa kutosha na wazazi wao kutokana na majukumu ya kila siku.
Watoto hao wamesisitiza kuwa wazazi wakikaa karibu nao, itawasaidia kupata msaada wa haraka wanapokutana na changamoto, ushauri na ulinzi, hali ambayo itawajenga kimaadili na kuwa na mustakabali bora kwa maisha.