SIMBA imefuzu raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya jioni ya leo kulazimishwa sare ya 1-1 na Gaborone United ya Botswana, lakini imepenya kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.
Kufuzu kwa Simba kumetokana na ushindi wa bao 1-0 ilioupata ugenini wiki iliyopita ambao kwa matokeo ya mechi ya leo iliyopigwa Kwa Mkapa imeibeba kwenda raundi ya pili na sasa itavaana na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini iliyoing’oa Simba Bhora ya Zimbabwe kwa penalti 4-2.
Timu hiyo ya Eswatini ilishinda leo nyumbani 1-0 ikilipa kisasi cha kulala ugenini 1-0 na mechi kwenda katika mikwaju ya penalti na wenyeji kuibuka kidedea na sasa itakuwa na kibarua mbele ya Mnyama katika mechi zitakazopigwa kati ya Oktoba 17-26. kuiotafuta makundi.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza likifungwa na kiungo mshambuliaji, Jean Charles Ahoua dakika ya 43 kwa mkwaju wa penalti iliyopatikana baada ya kiungo Morice Abraham kuangushwa eneo la hatari.
Bao hilo lilitosha kuzipeleka timu hizo mapumziko, huku wenyeji wakiwa mbele likiwa ndio shambulizi kubwa ambalo wekundu hao walilifanya katika kipindi hicho cha kwanza.
Gaborone United ilionyesha imekuja kikazi kutaka kupindua matokeo, ambapo iliishambulia zaidi Simba kipindi cha kwanza.
Kiungo mshambuliaji wa Gaborone Thatayaone Kgamanyane atajilaumu kwa nafasi mbili kubwa alizopoteza dakika ya 23 na 38 akiwa uso na kipa wa Simba Moussa Camara lakini akashindwa kumfunga
Katika kipinid cha pili Gaborone ilifanikiwa kusawazisha bao dakika ya 66 pia kwa penalti, mfungaji akiwa ni Lebogang Litselebaada baada ya winga wa timu hiyo, Thabo Maponda kuangushwa eneo la hatari na beki Chamou Karaboue.

LE 03
Maponda ndiye aliyekuwa mwiba kwa Simba tangu aingie mwanzoni mwa kipindi cha pili akichukua nafasi ya Sheikh Sesay ambapo kasi yake ilikuwa mwiba mkali kwa wenyeji
Kipindi cha pili Gaborone bado ikiendelea kuliandama lango la Simba ambapo Maponda alipoteza nafasi kubwa dakika ya 73 akishindwa kumalizia nafasi aliyotengeneza mwenyewe akishindwa kumfunga Camara.

Ahoua atajilaumu kwa kushindwa kuipunguzia nafasi Simba kwa nafasi zake dakika ya 67 na 79 akimtoka mpaka kipa lakini akashindwa kutulia na kufunga.
Simba imeungana na timu nyingine za Tanzania zilizofuzu raundi ya pili ikiwamo Yanga, Singida BS na KMKM na kwa sasa Azam ipo uwanjani kuumana na Al Merreikh Bentiu yua Sudan Kusini huku ikiongoza kwa bao 1-0 mbaloi na ushindi wa 2-0 iliyopata ugenini wiki iliyopita.