Azam yafanya kweli, yazifuata Simba, Yanga

MABAO mawili katika kila kipindi katika pambano la marudiano la Kombe la Shirikisho Afrika lililomalizika jioni hii, yametosha kuivusha Azam FC kwenda raundi ya pili ya michuano ya kimataifa ikizifuata Simba, Yanga, Singida BS na KMKM zilizotangulia mapema.

Azam iliifyatua El Merreikh ya Sudan Kusini kwa mabao 2-0 katika mechi  iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi na kuifanya ifuzu kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-0 kwani mechi ya mkondo wa kwanza ugenini ilishinda pia 2-0.

Beki wa kati, Yoro Diaby aliitanguliza Azam katika kipindi cha kwanza kwa bao la dakika ya 16 kabla ya Nassoro Saadun kufunga jingine sekunde chache kabla ya kumalizika kwa kipindi cha pili cha  pambano hilo ikimfanya kocha Florent Ibenge kuendeleza moto alionao katika michuano ya CAF.

Ibenge alitua Azam mwanzoni mwa msimu huu akitokea Al Hilal ya Sudan ambayo aliifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita.

AZA 01


Kwa matokeo hayo Azam sasa inatarajiwa kuvaana na KMKM katika mechi za raundi ya pili zitakazopigwa kati ya Oktoba 17-26 ili kusaka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo iliyoasisiwa mwaka 2004 kwa jina la Mzizima.

KMKM iliitoa As Port ya Djibouti kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-2, ikishinda 2-1 nje ndani, mechi zote zikipigwa visiwani Zanzibar.

Katika mechi ya jioni ya leo Azam itajilaumu kwa kushindwa kutoka na kapu na mabao kutokana na kuikimbiza Al Merreikh ambapo washambuliaji wa Azam wakiongozwa na Japhte Kitambala, Hamdi Barakat na Abdul Suleiman ‘Sopu’ sambamba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ walishindwa kutumia nafasi.

Azam inakuwa timu ya tano ya Tanzania kwa msimu huu kutinga raundi ya pili ya michuano ya CAF baada ya awali KMKM ya Zanzibar kutangulia katika Kombe la Shirikisho kama ilivyokuwa kwa Singida Black Stars, huku Yanga na Simba zikipenya Ligi ya Mabingwa.

AZA 02


Mlandege iliyokuwa ikishiriki pia Ligi ya Mabingwa ndio pekee iliyotolewa licha ya jana kushindwa kwa mabao 3-2 mbele ya Insurance ya Ethiopia, kwni kipigo cha 2-0 ilichopewa ugenini wiki iliyopita iliwafanya Wahabeshi kusonga mbele kwa jumla ya mabao 4-3.