Samia aahidi Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji, viwanda

Pwani. Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan amesema akipata ridhaa ya miaka mitano mingine Serikali yake itajenga Bandari ya Bagamoyo na kuifanya Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji na viwanda nchini.

Samia amesema hayo leo Jumapili Septemba 28, 2025 wakati akihutubia mkutano wa kampeni mkoani Pwani katika Uwanja wa Mkuza wilayani Kibaha.

Akizungumza mbele ya umati uliojitokeza kwenye kampeni hizo, Samia amesema endapo atapata ridhaa ya miaka mitano mingine Serikali itatekeleza na kusimamia mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo utakaoufanya Mkoa wa Pwani kuwa kitovu cha usafirishaji nchini na kuongeza fursa za biashara na ajira.

Bandari hiyo itakayojengwa eneo la Mbegani  itakuwa na gati za kisasa na ndefu zitakazokuwa na uwezo wa kupokea meli kubwa zaidi ya zinazopokewa Bandari ya Dar es Salaam.

Amesema bandari hiyo itaunganishwa kwa reli ya kisasa (SGR) kwa kipande cha kilomita 100 kutoka Bandari Kavu ya Kwala hadi bandarini hapo.

“Bandari hii itajengwa sambamba na eneo maalumu la kiuchumi la hekta 9,800 litakalochochea uzalishaji na kuvutia uwekezaji wa viwanda.

“Tumekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa bandari na eneo hili la biashara, tunaenda kutekeleza mradi huu kwa ushirikiano na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Shirika la Reli Tanzania (TRC) na sekta binafsi kwenye upande wa kongani za viwanda,” amesema Samia.

Kuhusu viwanda, Samia ameahidi kuendeleza ukuzaji wa viwanda Mkoa wa Pwani ambao ameutaja kuongoza  kwa kasi ya maendeleo ya viwanda.

Takwimu zinaonesha mwaka 2020 Pwani ilikuwa na viwanda 1,387  sasa vimefikia 1,631 ikiwa ni sawa  na ongezeko la viwanda 244 ndani ya miaka minne wastani wa viwanda 61 kwa mwaka.

Katika kipindi hicho vimejengwa viwanda vikubwa vipya 97 na kufanya jumla ya mkoa huo kuwa na viwanda 156 sawa na ongezeko la viwanda saba vikubwa kila mwaka.

Kwenye upande wa viwanda vya kati vimejengwa 81 katika miaka mitano na kufanya kuwa na jumla ya viwanda vya kati 191 ndani ya mkoa huo wastani wa viwanda 26 kila mwaka.

Amesema viwanda hivyo vimetoa ajira za moja kwa moja zaidi ya 21,000 na zisizo za moja kwa moja 60,000.

“Uwekezaji unaofanyika Pwani na kote nchini umeiwezesha nchi yetu kupiga hatua katika uelekeo wa kujitegemea kimapato na kibidhaa hasa za ujenzi ikiwamo mabati, marumaru, vioo na saruji,” amesema Samia.

Katika sekta ya maji, ameahidi miradi minne yenye thamani ya Sh44 bilioni katika mkoa huo itakayoongeza upatikanaji wa huduma hiyo  ambayo imefikia asilimia 89.

Mgombea huyo amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi Oktoba 29 kwa ajili ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM.

“Nataka twende na kauli mbiu ya ‘Twende Pamoja’ ikiwa na maana utakapoamka mpitie jirani yako, kama wewe ni balozi wa nyumba 10 wapitie watu wako wote muende mkapige kura,” amesema Samia.

Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amewaomba Watanzania kutofanya makosa ya kuchanganya viongozi wa vyama mbalimbali kwa kuwa madhara yake yanafahamika.

Amesema katika kipindi cha miaka minne, uongozi wa Samia umeweza kuzikabili changamoto za wakazi wa Mkoa wa Pwani, hivyo hawana cha kumlipa zaidi ya ushindi wa kishindo.


Kikwete amesema Mkoa wa Pwani utampa kura za kishindo mgombea huyo na wagombea wengine wa CCM, hivyo ni vyema nchi nzima wakafanya hivyo ili kumrahisishia utendaji wake.

“Kama Bunge linalomalizika sasa, wabunge wote ni wa CCM na linalokuja kutoka Pwani wabunge wote watakuwa CCM na naamini nchi nzima itakuwa hivyo.

“Pia, tutakuletea madiwani wa CCM ili halmashauri za wilaya na miji zote  ziwe chini ya chama chetu,  hatuko tayari kuchanganya pumba na mchele. Tunayajua madhara yake na hatutathubutu kufanya hivyo,” amesema Kikwete.

Kikwete ametumia fursa hiyo kumpongeza Samia kwa kuiongoza vyema nchi na kuifanya kuwa na mshikamano wa kitaifa.

“Umeiongoza nchi yetu vizuri, wewe ni mama mwema unajali changamoto za wananchi unaowaongoza na mwepesi kuchukua hatua. Nchi ni tulivu, maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanapatikana na yanaonekana.

“Nchi yetu yenye makabila 120 lakini bado imeendelea kuwa na umoja. Muungano wetu ni imara na bado unaendelea kuwa mfano kwa Afrika na mataifa mengine,” amesema.

Mwenyekiti wa CCM Pwani, Mwinshehe Mlao amesema pembejeo za ruzuku zilizotolewa kwa wakulima wa mkoa huo zimeondoa utofauti wa walionacho na wasionacho.

Amemuomba Samia kuongeza msukumo wa ujenzi wa Barabara ya Mbagala-Kongowe kwa kuwa inawaletea adha wakazi wa Mkoa wa Pwani.

“Ile barabara inatuhusu wakazi wa Pwani,  imekuwa kero, tayari mkandarasi yupo kazini lakini ombi letu aongeze kasi kutuondolea adha,” amesema Mlao.

Mratibu wa Kampeni Mkoa wa Pwani, Halima Mamuya amemuhakikishia mgombea wa urais kuwa, mkoa huo utaongoza kwa kura nyingi zitakazomuwezesha kupata ushindi wa kishindo.

Mgombea ubunge viti maalumu Mkoa wa Pwani, Hawa Chakoma  amesema wananchi wa mkoa huo wana kila sababu ya kuchagua CCM kutokana na maendeleo yaliyofanyika.

Mgombea ubunge wa Kibaha Vijijini,  Abuu Jumaa amesema ana uhakika mkubwa wa chama chake kushinda katika ngazi zote kwenye uchaguzi huo kutokana na kazi nzuri iliyofanywa.

“Nikisema tutashinda sio kwa kubabaisha, tutashinda kwa kasi, nawashangaa wanaopiga kelele kwenye mitandao sisi hatuchagui viongozi kwa kelele za mitandaoni bali maendeleo na kazi inayoonekana.

“Kibaha Vijijini tumepata fedha nyingi za miradi ya maendeleo zilizotumika kuanza ujenzi wa stendi ambayo hata hivyo, bado haijaisha tunaomba utuwezeshe kukamilisha ujenzi huu,tunaomba pia Kibaha Vijijini tupate mamlaka kamili,” amesema.

Mgombea ubunge wa Kibaha Mjini, Sylveste Koka amesema licha ya Samia kuipokea nchi ikiwa katikati ya mdororo wa uchumi wa kidunia na janga la Uviko-19 amefanya kazi kubwa kuhakikisha sasa uchumi umesimama na kuimarika.

“Tunajivunia Kibaha kuwa manispaa, wakati unaingia madarakani mapato ya halmashauri yalikuwa Sh5 bilioni lakini sasa yamefikia Sh21 bilioni. Tumepata shule mpya, zahanati, vituo vya afya, barabara na hivi karibuni tumesaini mkataba wa kujenga soko la kisasa,”amesema.

Mbunge huyo ametumia fursa hiyo kuomba barabara ya njia nane iliyojengwa kutokea Dar es Salaam isogezwe hadi Mlandizi ili kupunguza msongamano wa magari katika Mji wa Kibaha na ameomba pia mradi wa magari ya mwendokasi ufike Kibaha.