Rukwa. Mwenge wa Uhuru umepokewa leo Jumapili Septemba 28, 2025 katika Kijiji cha Kizi, Kata ya Paramawe mkoani Rukwa ambako utakimbizwa kwa kilomita 653.1, huku ukizindua miradi saba ya maendeleo, kuwekea mawe ya msingi miradi 15 na kukagua mingine 12.
Shughuli za mapokezi ya Mwenge huo ukitokea mkoani Katavi, zimehudhuriwa na viongozi wa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, pamoja na wananchi.
Akizungumza baada ya kuupokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Nyerere amesema mbio hizo zitadumu kwa siku nne na utakimbizwa katika wilaya tatu zenye halmashauri nne.
Halmashauri hizo ni Manispaa ya Sumbawanga na halmashauri za wilaya za Nkasi, Kalambo na Sumbawanga.
“Katika kipindi chote hicho, Mwenge utatembezwa kwenye jumla ya miradi 34 ya maendeleo pamoja na klabu nane,” amesema Makongoro na kuongeza kuwa miradi hiyo ina thamani ya Sh55.3 bilioni.
Kwa mujibu wake, katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi pekee, Mwenge utakimbizwa kwa umbali wa kilomita 153 na utapitia miradi minane yenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.
Mkuu huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kuhamasisha wananchi kushirikiana na Serikali katika kulinda miradi ya maendeleo na kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya na malaria.

“Ni wajibu wetu kushirikiana katika mapambano dhidi ya rushwa, dawa za kulevya na malaria. Tujali pia afya zetu kwa kuzingatia aina ya chakula tunachokula ili kuboresha lishe na kuimarisha ustawi wa jamii,” amesisitiza.
Aidha, amewataka wananchi kuutumia Mwenge wa Uhuru kama chachu ya mshikamano wa kitaifa na mwendelezo wa jitihada za kujiletea maendeleo kupitia miradi inayozinduliwa au kukaguliwa.