Dar es Salaam. Dar es Salaam. Wakati Chama cha Wananchi (CUF) kikiibua tuhuma dhidi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kukusanya kadi za mpiga kura, chama hicho tawala kimeibuka kikisema hakuna ukweli wowote dhidi ya madai hayo.
Malalamiko hayo yametolewa leo Jumapili, Septemba 28, 2025 na Mgombea Ubunge wa Newala Vijijini, Mneke Saidi, alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Saidi ambaye pia ni Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Newala Vijijini, amesema vitendo hivyo vinapingana na falsafa ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan na ahadi yake ya kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.
Kwa mujibu wa Saidi, CCM kinakusanya kadi hizo kwa madai ya kuzihakiki, si Newala pekee bali pia mikoa ya Kigoma na Tabora.
Alinukuu maneno yaliyoandikwa nyuma ya kadi ya mpiga kura yanayosema kadi hizo ni mali ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi na hairuhusiwi kufanyiwa mabadiliko wala kukabidhiwa mtu asiyeruhusiwa.
“CCM wameamua kwa makusudi, wakishirikiana na baadhi ya maofisa wa Tume ya Uchaguzi na vyombo vya ulinzi, kuuvuruga uchaguzi huu. Hii ni kinyume na dhamira ya Rais Samia kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki,” alisema.
Saidi alieleza kuwa tayari Septemba 9 aliripoti suala hilo Polisi na siku iliyofuata, Msajili wa Vyama vya Siasa aliitisha kikao cha viongozi wa vyama wilayani Newala na CCM walipewa onyo. Hata hivyo, amesema vitendo hivyo vimeendelea na Septemba 20, 2025, Polisi walikamata viongozi wawili wa CCM katika Kijiji cha Nyakahako wakiwa na kadi nyingi, lakini baadaye walitolewa kituoni bila kufikishwa mahakamani.
Akijibu tuhuma hizo alipozungumza na Mwananchi kwa simu, Katibu wa CCM Wilaya ya Newala, Robert Mwega amekanusha madai hayo na kusema Saidi anatafuta visingizio baada ya kuona dalili za kushindwa.
“Hizo tuhuma hazina ukweli wowote. Huyo mpinzani anatapatapa tu. Wananchi wampuuze kwa kuwa sisi CCM tumekuwa tukifanya kampeni kwa kistaarabu na kuitangaza ilani yetu yenye matumaini,” almesema Mwega.
Mwananchi pia imezungumza na Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Newala, Friday Sondasy ambaye amekiri kupokea malalamiko hayo lakini akasema ofisi yake haina mamlaka ya kukamata watu, hivyo jukumu hilo liliachwa kwa Jeshi la Polisi.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Issa Suleiman amekiri kukamatwa kwa watuhumiwa wawili katika tukio hilo, lakini akasema wako nje kwa dhamana na uchunguzi bado unaendelea.
“Ni kweli tulipokea malalamiko na kuwakamata watuhumiwa wawili. Kwa sasa wako nje kwa dhamana na Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza ili kubaini ukweli wa jambo hili,” amesema.
Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma wa CUF, Mohamed Ngulangwa ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kuchukua hatua madhubuti za kisheria dhidi ya viongozi wa CCM wanaodaiwa kuendesha shughuli hiyo.
“Tunamuomba Katibu Mkuu wa CCM kuwaagiza viongozi wake kusitisha mara moja kazi hiyo haramu na kuwarejeshea wananchi kadi zao. Vinginevyo sisi tuko tayari kupambana kisiasa, lakini kwa nini CCM wameamua kuweka mpira kwapani?” amehoji Ngulangwa.
Aidha, CUF kimeomba Rais Samia Suluhu Hassan kuchukua hatua dhidi ya wasaidizi wake ndani ya Serikali na CCM wanaodaiwa kuhujumu dhamira yake ya kufanikisha uchaguzi huru na wa haki.