Mgombea udiwani CCM aahidi kukomesha wanafunzi kutembea umbali mrefu

Moshi. Mgombea udiwani wa Kata ya Karanga kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Deogratius Mallya, ameahidi kushughulikia changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni kwa kuhakikisha ujenzi wa shule mpya ya sekondari katika kata hiyo, akitachaguliwa kuwa diwani.

Akizungumza leo, Septemba 28, wakati wa uzinduzi wa kampeni zake uliofanyika katika kata hiyo, Mallya amesema shule nyingi zipo mbali na makazi ya wananchi, jambo linalowalazimu wanafunzi kutembea hadi kilomita tano kila siku kwenda na kurudi shuleni.

“Hali hii inawaathiri kitaaluma kwani hufika shuleni wakiwa wamechoka na mara nyingine huchelewa. Nitahakikisha tunapata suluhisho la kudumu ili watoto wetu wapate elimu katika mazingira rafiki,” amesema Mallya.

Amesema kuwa shule hiyo mpya itajengwa pembezoni mwa Chuo cha Ufundi Karanga, akisisitiza kuwa ni mradi muhimu kwa maendeleo ya elimu katika kata hiyo.

Aidha, Mallya ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara kwa kiwango cha lami ili kuhakikisha zinapitika nyakati zote na kurahisisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Karanga.

“Nawaahidi, endapo mtanirudisha madarakani, nitahakikisha barabara zote ndani ya kata zinaunganishwa kwa kiwango cha lami kwa kushirikiana na mamlaka husika.

“Naomba mnitume tena. Karanga mpya inawezekana sana, tuliwapa wapinzani nafasi kwa miaka 15, lakini leo ukiuliza walichofanikisha, hakuna majibu ya kuridhisha,” amesema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amewahakikishia wananchi kuwa, endapo atachaguliwa, atasimamia uwepo wa mwanasheria katika ofisi ya mbunge ambaye atatoa elimu ya kisheria kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili wapate mikopo ya halmashauri kwa mujibu wa sheria na kanuni.

“Nataka niwaahidi, Oktoba 29 mkishanichagua, tutaweka mwanasheria katika ofisi ya mbunge, atakuwa msaada kwa vikundi vyote kuwaandikia mikataba, kuwashauri kisheria na kuwasaidia kupata mikopo,” amesema Shayo.

Kuhusu watu wenye ulemavu, Shayo amesema hatowalazimisha kujiunga na vikundi ili kupata mikopo, bali atahakikisha wanapatiwa fedha moja kwa moja.

Pamoja na mambo mengine, Shayo ameahidi kununua magari mawili aina ya Costa kwa matumizi ya kijamii, kama vile misiba na harusi, ambayo yatatolewa bure kwa wananchi.

“Hizi gari nitazinunua kwa fedha zangu mwenyewe. Baada ya Oktoba 29, mkishanipa kura za kutosha, mtakuwa huru kupiga simu ofisi ya mbunge mnapokuwa na dharura yoyote, iwe ni harusi, msiba au mgonjwa. Magari haya yatakuja kuwasaidia bila gharama yoyote,” amesema.

Amesema kuwa lengo lake ni kuhakikisha ofisi ya mbunge inakuwa ya msaada wa moja kwa moja kwa wananchi, hasa nyakati za uhitaji mkubwa.