Wizara ya Madini yafikia asilimia 98 lengo la ukusanyaji mapato

Geita. Naibu Waziri Mkuu Doto Biteko amesema mageuzi ya teknolojia na usimamizi madhubuti katika sekta ya madini, yameiwezesha serikali kukusanya sh3.8 trilioni katika kipindi cha miaka minne, sawa na asilimia 96 ya lengo la Wizara ya Madini.

Akizungumza wakati wa kufunga monyesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini Dk Biteko amesema mabadiliko hayo yamejidhihirisha zaidi kwa wachimbaji wadogo, ambao mchango wao umeongezeka kutoka asilimia 20 mwaka 2020 hadi asilimia 40 mwaka 2024, huku mapato yao yakiongezeka kutoka asilimia 6.8 hadi asilimia 10 katika kipindi hicho.

Amesema katika Mkoa wa Geita pekee, wachimbaji wadogo wamezalisha kilo 22,000 za dhahabu zenye thamani ya Sh trilioni 3.43 na kuiingizia serikali mapato ya zaidi ya Sh2.5 bilioni kati ya mwaka 2021 na 2025.

Kutokana na mafanikio hayo, serikali imeanzisha masoko ya madini 43 na vituo vya ununuzi 109 ili kurahisisha biashara na kuongeza ushiriki wa Watanzania katika mnyororo wa thamani kuanzia utafiti, uchimbaji, uchenjuaji hadi biashara.

Amesema katika kukuza sekta hiyo na kuongeza thamani ya madini yanayozalishwa , viwanda nane vya uchenjuaji na usafishaji madini vimeanzishwa nchini kwa ajili ya dhahabu, shaba na nikeli, hatua inayolenga kuongeza thamani ya madini ndani ya nchi.

Aidha serikali imesisitiza ajira zinazotolewa na makampuni ya madini ziwe na mshahara sawa kati ya Watanzania na wageni, ikikemea tabia ya baadhi ya kampuni kuwalipa Watanzania kidogo licha ya kufanya kazi sawa na wageni.

 “Kweli ajira zimetolewa kwa watanzania sasa tuangalie mishahara ya hawa watanznaia iko sawa isiwe hii asilimia tano ya wageni wanalipwa zaidi huku kazi kubwa ikifanywa na wazawa,”amesema Biteko

Ushirikiano wa wadau waanza kuzaa matunda
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amesema maonyesho hayo yamefungua fursa kwa wachimbaji na wafanyabiashara kupata elimu kuhusu masoko, afya na usalama kazini.

Akizungumzia upatikanaji wa leseni kwa wachimbaji wadogo,Shigela amesema zimeongezeka kutoka 1000 hadi kufikia 9000 ambazo zimetolewa katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Shigela ameiomba serikali kutengeneza sheria itakayowawezesha wachimbaji badala ya kuhifadhi fedha wahifadhi dhahabu kupitia Benki kuu nchini (BOT).

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, akiwa katika banda la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) wakati wa hafla ya kufunga Maonesho ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika katika Viwanja vya  Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita kuanzia Septemba 18 – 28 2025.



Amesema miaka mitatu iliyopita kilo moja ya dhahabu iliuzwa Sh160 milioni lakini sasa imepanda hadi kufikia Sh300 na kuiomba serikali kufungua wigo ili wachimbaji wenye uwezo wahifadhi dhahabu badala ya fedha.

Aidha ameiomba serikali kuweka msamaha wa kodi kwa bidhaa zinazoondoa matumizi ya zebaki na kutolewa ruzuku kwa bidhaa mbadala ili kuondokana na matumizi ya zebaki ambayo yanaathiri afya na mazingira.

Meneja mawasiliano kutoka benki Kuu (BOT) Victoria Msina amesema hadi sasa benki hiyo imenunua tani 10 za madini yenye thamani ya Sh2.5 trilioni.

Amesema mbali na kukusanya dhahabu pia benki hiyo huhamasisha wachimbaji wadogo kujiunga pamoja ili waweze kupatiwa mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha.

Aidha amewataka wachimbaji kuwekeza kwenye dhamana za serikali na kuwataka wakope kwa malengo ili waweze kuona tija ya kazi wanazofanya.


Meneja wa benki ya CRD kanda ya Mangharibi amesema benki ya CRDB Foundation inatoa mitaji wezeshi kwa vijana na kina mama ambapo wametumia amonyesho hayo kwa kupita migodini na kukutana na kina mama na kuwaeleimisha.

Amesema hadi sasa Sh90 bilioni zimetolewa kwa wachimbaji na Wafanyabiashara wa madini na kupitia chama cha wachimbaji wanawake(Tawoma) wameingia makubaliano ya kuwawezesha kupata mitaji wezeshi pamoja na mitambo ili waweze kufanya kazi kwa tija.