………….
Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara wa Hungary, Mhe. Péter Szijjártó amewasili nchini Septemba 29, 2025 kwa ziara ya kikazi ya siku moja.
Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Mhe. Szijjártó’ amepokelewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi na viongozi wengine waandamizi kutoka Serikalini.
Akiwa nchini, Mhe. Szijjártó’ atakutana kwa mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo kabla ya kuwa na mkutano wa pamoja na Waandishi wa Habari.
Kadhalika wakati wa ziara yake ambayo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na Hungary, Mawaziri hao watashuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Serikali Mbili kuhusu Mradi wa Usambazaji Maji katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, Hati ya Makubaliano kati Kampuni ya MeOut ya Hungary na Kituo cha Kidijitali cha Tanzania kuhusu masuala Ubunifu na kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano kati ya MeOut na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo ya Tanzania.
Aidha, Mhe. Szijjártó’ kwa pamoja na Mhe. Balozi Kombo watashiriki katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Dar es Salaam ya Ubalozi wa Hungary uliopo jijini Nairobi, Kenya.
Hii ni ziara yake ya pili nchini ambapo ziara yake ya kwanza ilifanyika mwezi Machi, 2024.