Juma Kaseja mguu sawa Championship

BAADA ya ratiba ya Ligi ya Championship kuwekwa wazi, Kocha wa Kagera Sugar, Juma Kaseja amesema moja ya malengo makubwa anayopambana nayo ni kuhakikisha anakirejesha tena kikosi hicho Ligi Kuu Bara, licha ya ushindani mkubwa uliopo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kaseja alisema baada ya ratiba kutoka na kikosi hicho kuanza mechi mbili mfululizo nyumbani, wanahitaji kupambana ili kupata pointi zote sita mapema, kabla ya kuanza kwenda ugenini ambako panakuwa ni pagumu zaidi.

“Kuanza nyumbani kwetu ni jambo nzuri lakini itapendekeza kama tukianza kwa ushindi mechi zetu zote mbili, Championship ni ngumu sana na ukiangalia kila timu imefanya usajili mzuri kutokana na malengo yake iliyojiwekea pia,” alisema Kaseja.

Kaseja aliyewahi kuichezea timu ya Taifa Stars na klabu za Simba na Yanga, alisema hadi sasa kikosi hicho kina zaidi ya wiki tatu mazoezini kikijiandaa na msimu wa 2025-2026 na hali ya wachezaji ni nzuri na wanaonyesha morali kikosini.

KASEJA Pict


Kagera itaanza kufungua pazia la Ligi ya Championship msimu wa 2025-2026 kwa mechi zote mbili nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba dhidi ya maafande wa Transit Camp Oktoba 10, kisha kuikaribisha, Barberian zamani Kiluvya United Oktoba 18.

Kipa huyo aliyeitumikia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, alijiunga nayo Machi 4, 2025, akichukua nafasi ya Mmarekani Melis Medo aliyeondoka Februari 25, 2025, baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa matokeo ya kikosi hicho.

Kagera iliyodumu Ligi Kuu Bara kwa miaka 20 tangu ilipoanza kushiriki 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-25, baada ya kushinda mechi tano tu, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15 na pointi 23.