Dar es Salaam. Mshtakiwa, Eric Ayo anayedaiwa kusafirisha vinyonga 164, nyoka na mijusi, amemwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) akiomba kufanya majadiliano ya kukiri makosa yake na apunguziwe adhabu.
Ayo na wenzake wawili wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi namba 23/2021 yenye mashtaka matatu yakiwamo ya kuongoza genge la uhalifu na kusafirisha nyara za Serikali pamoja na kutakatisha fedha, linalomkabili Ayo peke yake.
Mshtakiwa ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu Septemba 29, 2025, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa kuwa amemuandikia barua DPP, akiomba kukiri mashtaka yake ili amalize kesi yake.
Awali, wakili wa Serikali, Winiwa Kasala aliieleza Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu kuwa kesi hiyo imeitwa kwa kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.
“Kutokana na upelelezi wa kesi hii kutokukamilika, tunaiomba Mahakama yako ipange tarehe nyingine kwa kutajwa,” ameomba Kasala.
Hakimu Magutu amekubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 13, 2025 kwa kutajwa.
Mbali na Ayo, washtakiwa wengine ni Ally Ringo na Aziz Ndago ambao kwa pamoja, wanadaiwa kusafirisha nyara hizo zenye thamani ya Sh20milioni bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyama Pori nchini.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kati ya Desemba mosi 2020 na Januari Mosi, 2021 mkoani Morogoro, Tanga na Dar es Salaam, kupanga na kuongoza genge la uhalifu kwa kukusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali bila kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini.
Shtaka la pili ni kukutwa na nyara za Serikali tukio wanalodaiwa kulitenda kati ya Desemba mosi, 2020 na Januari Mosi, 2021 maeneo ya Tanga, Morogoro na Dar es Salaam.
Inadaiwa katika kipindi hicho, washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakikusanya, kusafirisha na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vinyonga 164, Mijusi 20 na nyoka 6, wote wakiwa na thamani ya Sh20 milioni, mali ya Serikali,
Pia washtakiwa hao wanadaiwa kukutwa na Dola 9,000 za Marekani (Sh19.8 milioni).
Shtaka la tatu ni la kutakatisha fedha linalomkabili Ayo, peke yake, Januari 26, 2021 katika benki ya CRBD iliyopo Msamvu mkoani Morogoro, kwa makusudi anadaiwa kubadilisha fedha Dola 400 za Marekani 400 na kupata Sh923,600, wakati akijua fedha hizo zilikuwa zimetokana na uuzaji wa nyara za Serikali.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Machi 16, 2021 na kusomewa mashtaka yanayowakabili.