Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe, upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Wakili wa Serikali, Winiwa Kassala, ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Jumata-tu Septemba 29, 2025, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28, yakiwemo kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha, huku mashtaka ya kutakatisha fedha ya-nayomkabili Mkondya pekee yake.
Hata hivyo, John, ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, yupo nje kwa dhamana baada ya kuomba dhamana Mahakama Kuu, na pia hana mashtaka ya kutakatisha fedha.
Kassala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu, anayesikiliza shauri hilo.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa leo kwa ajili ya kutajwa na upelelezi upo katika hatua za mwisho kukamilika, hivyo tunaomba Mahakama itupangie tarehe fupi kwa ajili ya kutajwa,” amesema Kassala.
Hakimu Magutu, baada ya kusikiliza taarifa hiyo, amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 9, 2025, kwa kutajwa.
Mkondya anaendelea kubaki rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walif-ikishwa Mahakamani hapo Novemba 5, 2024, na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 31523 ya mwaka 2024.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28, mashtaka 19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka 9 ni ya kutakatisha viwanja. Katika mojawapo ya mashtaka ya kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari Mosi, 2020, na Desemba Mosi, 2023, jijini Dar es Sa-laam, walitenda makosa hayo.
Inadaiwa kuwa Mkondya, akiwa mkurugenzi wa kampuni hiyo, na John akiwa mkaguzi wake, waliendesha biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi tatu zaidi ya waliyotoa. Washtakiwa hao wanadaiwa kuiji-patia Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa ku-waahidi kupata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.
Katika mashtaka tisa ya utakatishaji fedha ya-nayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari mosi, 2020, na Desemba Mosi, 2023, akiwa katika mkoa wa Dar es Salaam na akiwa Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, alijipatia jumla viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB, eneo la Idunda mkoani Njombe.
Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua kuwa ni mali iliyoletwa na makosa ya awali ya kuendesha biashara ya upatu.