Dar es Salaam. Mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameahidi ujenzi wa masoko 13 katika Wilaya ya Ubungo yatakayochochea uchumi wa wananchi na Taifa.
Aidha, amewaahidi wafanyabiashara ndogondogo wa Ubungo jijini Dar es Salaam kwamba biashara zao zitarasimishwa ili kuwawezesha kupata mikopo na kupunguza urasimu wa kupata leseni.
Mgombea mwenza huyo amesema hayo leo Jumatatu, Septemba 29, 2030 katika mkutano wa kampeni uliofanyikia Uwanja wa Mabibo Hostel, (EPZA) Wilaya ya Ubungo yenye majimbo mawili ya Ubungo na Kibamba.
Dk Nchimbi amesema katika miaka mitano ijayo, wanakwenda kurasimisha biashara ndogondogo ili wafanye kihalali na kuwawezesha kupata mikopo na wafanye bishara ziwe zenye tija na upataji leseni kwa kupunguza urasimu.

“Kujenga na kukarabati masoko mapya 13, nimeambiwa watu wanakwenda sana Mlimani City, kituo cha Kimataifa cha Afrika Mashariki kwa sababu ya miundombinu mizuri, tumesema miundombinu hii inapaswa kuwa kwenye masoko mengine ili watu wayapende,” amesema Dk Nchimbi.
Ahadi hizo amezitoa akirejea kile kilichoelezwa na mgombea ubunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo ambaye amesema biashara wilayani humo yenye majimbo ya Ubungo na Kibamba zimeongezeka kutoka 4,022 mwaka 2020 hadi 8,997.
Miongoni mwa biashara hizo ni za migahawa, saloon, bodaboda, nyumba za kulala wageni pamoja na ‘Mini Supermarket’ ambapo Profesa Kitila amesema wamewafikia kwa kuwasikiliza changamoto zao na jinsi ya kuzitatua.
Kuhusu suala la usafiri, Dk Nchimbi amesema wao kama chama wanakiri kumekuwa na changamoto ya usafiri na usafirishaji katika Jiji hilo na kadhia hiyo inatokana na uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia kufanya maboresho makubwa ya miundombinu ya barabara.
Amesema hatua hiyo imesababisha usumbufu wa muda lakini mwisho wa wanaboresho hiyo adha ya usafiri na usafirishaji katika jiji hilo kubwa la kibiashara iwe imemalizika.
Dk Nchimbi amegusia usafiri wa mabasi yaendayo haraka akisema:”
Tumekuwa na sera ambazo si nzuri, utaratibu wa sasa Serikali inajenga miundombinu, inanunua mabasi, hii tumeona haina tija, Serikali imetengeneza sera ambazo sasa itajenga miundombinu lakini ununuzi wa mabasi itafanywa na sekta binafsi.”

Amesema Serikali ikifanya na sekta binafsi tija inaongezeka kwani sekta binafsi inataka kupata faida. Ametolea mfano, barabara ya mwendokasi Kimara- Moroco- Kivukoni- Gerezani: “Tayari yameagizwa mabasi mapya 177 ambayo yatakuja kupunguza changamoto hiyo.”
Ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika mradi huo tayari umeanza kutekelezwa kwani Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) Gerezani hadi Mbagala imekabidhiwa Kampuni ya wazawa ya Mofat.
Maboresho sekta ya afya, maji
Dk Nchimbi amewaambia wana Ubungo kwamba miaka mitano ijayo wanakwenda kuiboresha zaidi Hospitali ya Manispaa kwa kuongeza majengo, watumishi na vifaa lengo huduma nyingi zitolewe hapo ili wananchi wa Ubungo wasiende mbali.
Kuhusu maji, amesema wanakwenda
kuviboresha vyanzo vya maji katika maeneo ya Kimara- Ubungo- Sinza na Makurumula pamoja na kuimarisha mfumo wa mawasiliano wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Dawasa) ili mwananchi wanapowasilisha malalamiko yafanyiwe kazi haraka.
Dk Nchimbi amempongeza Rais Samia jinsi alivyodhibiti mfumuko wa bei akitolea mfano Agosti 2025, mfumuko ulikuwa asilimia 3.1 wakati nchi ya Malawi ulikuwa asilimia 28.

“Hakuna eneo muhimu kama kusimamia ukuaji wa uchumi … katika jambo hili lazima wana CCM, Watanzania tuone umuhimu wa Rais Samia,” amesema Dk Nchimbi.
Pia, amesema Rais Samia amekuza diplomasia ya uchumi: “Kupitia Balozi zetu, Rais amekuza na kuvutia wawekezaji wengi, kupata fedha za kigeni na kuuza nje bidhaa zetu. Kiwango tunachouza Kenya ni kikubwa kuliko tunachonunua.”
Tuone fahari tunapojitambulisha na Rais Samia,” amesema Dk Nchimbi.
Alichokisema Profesa Kitila
Awali, mgombea ubunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo amesema Ubungo ina biashara zaidi ya 8,000 kutoka 4,022 mwaka 2020.
Profesa Kitila ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kamati iliyoandika Ilani ya CCM 2025/2030 amesema wamekwenda kuzungumza na makundi mbalimbali Jimbo la Ubungo kujua matarajio yao.
Amesema wanaona haja ya kupanua na kuboresha mitaji kwa wafanyabiashara na mafunzo kwa wajasiriamali ili waweze kufanya vizuri biashara zao.
Profesa Kitila ambaye pia ni Waziri wa Mipango na Uwekezaji amesema katika mikutano hiyo na makundi hayo wamezungumzia tatizo la maji na wao wakazungumza na Dawasa jinsi ya kutatua changamoto hiyo.
Amesema wamezungumzia kamatakamata na kufukuzwa kwa wafanyabiashara: “Nimewaahidi katika wilaya ya Ubungo yenye majimbo ya Ubungo na Kibamba kwamba wafanyabiashara ndogondogo hawatabughudhiwa.”
Profesa Kitila amesema amezungumza na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) kwamba barabara zinazojengwa waweke barabara za akiba kwa ajili ya wafanyabiashara ndogondogo wakiwemo mama lishe kama ambayo huacha kwa ujenzi wa vituo vya mafuta.
Pia, amesema ameahidi kujenga kituo kipya cha afya Manzeze, kupandisha hadhi kituo cha Mavurunza iwe Hospitali ya Wilaya.
Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa UWT, Mary Chatanda amesema nimewaambia wanawake wapunguze magomvi na wanaume wao kwani kazi iliyopo mbele ni kutafuta ushindi wa Samia.
“Mmeo akirudi mwambie haloo bebi, kwa hiyo tumalize magomvi na waume zetu na tupambane kutafuta kura za Mama Samia, wabunge na madiwani,” amesema Chatanda.