Othman ataja mambo manne yatakayompa urais Zanzibar

Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar (ACT Wazalendo), Othman Masoud Othman, ameyataja mambo manne ambayo ni siri ya ushindi wa chama chake katika nafasi ya urais visiwani humo katika uchaguzi wa mwaka huu, huku akijinasibu kuwa, tayari chama hicho kimeshayatimiza.

Miongoni mwa siri hizo, kwa mujibu wa Othman ni kujua wanachokipambania ambacho ni masilahi ya Wazanzibari, hali halisi ya Zanzibar iliyogubikwa na ugumu wa maisha na umasikini, fikra za ushindi walizonazo wanachama wa chama hicho na kuzijua mbinu za washindani wao.

Ametaja hayo leo Jumatatu Septemba 29,2025 wakati wa uzinduzi wa timu ya ushindi kwa upande wa Unguja. Uzinduzi huo ulihusisha timu za ushindi za chama hicho kuanzia ngazi ya mkoa, majimbo, matawi na shehia zitakazokuwa na jukumu la kutafuta kura ili ushindi kupatikana.


Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, amezindua timu hizo, sambamba na kuzikabidhi vitendea kazi ikiwemo magari saba ili kurahisisha majukumu yao ya kila siku hadi kufikia Oktoba 29,2025.

Mgombea huyo, amesema ufundi kwenye mapambano yoyote kanuni ya kwanza lazima ujue unapambania nini? au unatafuta kitu gani, jambo ambalo ACT Wazalendo kinajua wanachokipambania kwa Wazanzibari.

“Hivi kuna mtu hajui tunapambania nini ACT? Tunayoyapambania yapo wazi ni Zanzibar kwanza, tunataka haki sawa katika Muungano. Ndani ya ACT Wazalendo, hatubuni bali tunaeleza mambo tunayoyaishi, akili yetu na ufahamu wetu upo wazi, tunajua tunachokipambania,”

“Kanuni nyingine, ukiingia kwenye mapambano jiulize hali halisi ilivyo sasa je, una sababu ya kupambana au kutaka mabadiliko? Jamani hali ilivyo kuna mtu anataka kuishi maisha haya? amehoji Othman na kujibiwa hakuna.


Katika ufafanuzi wake, Othman amedai hali ya maisha ya Wazanzibari si nzuri, huku Serikali ikijikita katika ujenzi wa  miundombinu ya madaraja na barabara, badala ya kuboresha maisha ya wananchi.

Othman amesema kanuni nyingine, ukienda katika mapambano, unapaswa kuangalia fikra na akili za washindani au mpinzani wako, jambo ambalo ACT Wazalendo wameshalifanya kwa kuwasoma na kujua mbinu zao.

“Kwa haya mambo ya leo, kama mtu huamini au una wasiwasi basi uonane na madaktari. Hivi mna wasiwasi na mwendesha mashtaka wa zamani? Mna wasiwasi na mwanasheria mkuu wa zamani au mna wasiwasi na OMO? amehoji Othman huku akijibiwa hakuna…

Mwenyekiti wa timu za ushindi ya Chama cha ACT Wazalendo, Ismail Jussa amesema timu hizo zinafanya kazi usiku na mchana za kuhakikisha Othman anapata kura za kishindo.

Jussa amesema ushindi wa ACT Wazalendo upo si kwa sababu ya ACT Wazalendo, bali uungwaji mkono wanaoupata kutoka kwa vyama mbalimbali visiwani humo.

“Hizi ni timu za kuitafutia ushindi Wazanzibari, naomba msiwakebehi CCM maana tupo jahazi moja, kinachotakiwa tuwazindueni,”.

“Najua kazi za timu hizi zimeshaanza, sasa kuanzia leo hakuna kulala tena,” amesema Jussa ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Zanzibar).

Mjumbe wa kamati kuu ya ACT Wazalendo, Juma Duni Haji ‘Babu Duni’ amewataka wananchi wa Zanzibar kukumbuka mambo matatu yakiwemo ya ugumu wa maisha na umaskini kabla ya kufanya uamuzi Oktoba 29 kwenye sanduku la kura.

Katibu wa Idara ya Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa ACT Wazalendo, Salim Biman amesema tukio hilo ni la kihistoria ili kufanikisha ushindi wa chama hicho katika uchaguzi wa Oktoba 29.

Katika hatua nyingine, Biman amesema mikutano ya kampeni za mgombea urais wa chama hicho, Othman itaendelea kesho Jumanne Septemba 30, kisiwani Pemba baada ya kumalizika raundi ya Unguja.

Naibu Katibu Oganaizesheni, Mafunzo na Wanachama, Khamis Ali Salim wa ACT Wazalendo, amesema timu hizo za ushindi ndio zitakazowezesha safari ya ushindi wa kishindo wa chama hicho ili kuinusuru Zanzibar.

“Timu hizi za ushindi zitaanza mafunzo wiki hii, tumemaliza mafunzo kwa timu ushindi za Pemba,” amesema Salim.