Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imekiamuru Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwasilisha mahakamani hapo nyaraka zinazohusiana na rasilimali zake kufuatia kesi ya mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali usio sawa kati ya Tanzania Bara na Zanzibar inayokikabili.
Amri hiyo imetolewa na Jaji Hamidu Mwanga anayesikiliza kesi hiyo, leo Jumatatu, Septemba 29, 2025 kufuatia maombi yaliyofunguliwa mahakamani hapo na walalamikaji katika kesi hiyo, huku mahakama hiyo ikikipa chama hicho siku 14 kutekeleza amri hiyo.
Wakati huohuo chama hicho kimeibua pingamizi lingine kikihoji mamlaka ya mahakama hiyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo ya msingi.
Kutokana na pingamizi hilo usikilizwaji wa kesi hiyo ya msingi umesimama kupisha usikilizwaji na uamuzi wa pingamizi hilo ambalo mahakama hiyo imepanga kulisikiliza Oktoba 30, 2025.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed, na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Walalamikaji wanadai kuwa kumekuwa na mgawanyo usio sawa wa mali za chama na rasilimali za kifedha kati ya Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara, kinyume na Sheria ya Vyama vya Siasa na Katiba ya chama hicho.
Pia wanadai kuwa kuna ubaguzi wa kidini na kijinsia; pamoja na kutoa maoni na matamko yaliyo na nia ya kuvuruga muungano kati ya pande mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kesi hiyo walalamikaji kupitia mawakili wao, Shaban Marijani, Gido Simfukwe na Alvan Fidelis, waliwasilisha shauri dogo wakiomba mahakama iwaamuru walalamikiwa wawapatie nyaraka mbalimbali zinazoonesha mali za chama na za vikao kuanzia mwaka 2019 mpaka 2024, wazitumie katika kesi hiyo.
Nyaraka hizo ni Tamko la Mwaka la Mali zinazomilikiwa na chama hicho; Taarifa za kifedha chama hicho zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Mihtasari ya vikao vya Bodi ya Wadhamini wa chama hicho.
Nyingine ni mihtasari yote ya Agenda za vikao vya Kamati Kuu ya chama hicho, mihtasari yote ya ajenda za vikao vya Kamati Maalumu ya Zanzibar, Mihtasari yote ya ajenda za vikao vya Sekretarieti ya Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema Zanzibar.
Vilevile Taarifa za Kibenki za akaunti namba 011103010075 yenye jina la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, iliyoko katika Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce Limited).
Wajibu maombi/walalamikiwa kupitia mawakili wao Dk Rugemeleza Nshalla, Hekima Mwasipu na Jerehemia Mtobesya walipinga maombi hayo.
Pamoja na mambo mengine wakidai kuwa waombaji hawakukidhi matakwa ya kisheria kustahili kupewa nyaraka hizo, huku pia wakikana kuwa nazo badala wake wakimtupia mpira Msajili wa Vyama vya Siasa na CAG kuwa ndio wanazo na ndio wanapaswa kuzitoa.
Jaji Mwanga katika uamuzi wake kwanza ametupilia mbali hoja za walalamikiwa kuwa hazikuwa na mashiko huko akikubaliana na hoja za walalamikaji.
Hata hivyo kati ya aina saba za nyaraka hizo walizoziomba, jaji Mwanga amewakubalia katika aina tatu tu za nyaraka hizo ambazo ndizo alizowaamuru wajibu maombi/walalamikiwa waziwasilishe mahakamani, huku akiwakatalia aina nne.
Nyaraka hizo ambazo mahakama hiyo imewaamuru walalamikiwa waziwasilishe mahakamani ni tamko la mwaka la mali zinazomilikiwa na chama hicho,
Nyingine ni taarifa za kifedha chama hicho zilizokaguliwa na Mdhibiti na CAG na Taarifa za Kibenki za akaunti namba 011103010075 yenye jina la Chama cha Demokrasia na Maendeleo, iliyoko katika Benki ya Taifa ya Biashara (National Bank of Commerce Limited).
Nyaraka zinazohusu agenda na mihtasari ya vikao Jaji Mwanga amewakatalia waombaji/walalamikaji pamoja na mambo mengine akisema kuwa hawakuainisha tarehe za vikao ambavyo walihitaji nyaraka zake na kwamba haiwezekani kuwapatia nyara zote kuwa kuna vikao vingine huwa ni vya siri ambazo hazipaswi kutolewa hadharani.
“Hivyo mahakama inakubaliana na maombi ya waombaji kwa kiwango kilichoelezwa na inawaamuru wajibu maombi kuwasilishwa mahakamani nyaraka hizo zilizoainishwa ndani ya siku 14 kuanzia tarehe ya uamuzi huu.”, amesema Jaji Mwanga na kubainisha kuwa nyaraka hizo zinapaswa kuwasilishwa mahakamani kabla au kufikia Oktoba 13, 2025.
Pia mahakama hiyo imewapa waombaji/walalamikaji siku tisa za kazi badala ya siku 21 walizoziomba, kuzipitia nyaraka hizo kabla ya siku usikilizwaji wa kesi, ambazo zinaishia Oktoba 24, 2025.
Hata hivyo baada ya mahakama kumaliza kutoa uamuzi huo, wakili Rugemeleza ameieleza mahakama kuwa pia wamewasilisha pingamizi lingine wakihoji mamlaka ya mahakama hiyo kusikiliza kesi hiyo.
Wakili Rugemeleza amebainisha kuwa pingamizi hilo linahusiana na muundo wa mahakama hiyo (yaani jaji mmoja) kuisikiliza kesi hiyo ambayo ina madai ya kikatiba.
Kutokana na pingamizi hilo, Jaji Mwanga amepanga kulisikiliza Oktoba 30, 2025.
Katika kesi ya msingi walalamikaji wanaomba Mahakama hiyo itamke kuwa wadaiwa wamekiuka kifungu cha 6A(1), (2), (5) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258 Marejeo ya mwaka 2019 na iwaelekeze wazingatie kifungu hicho.
Pia wanaiomba Mahakama hiyo itamke kwamba ugawaji wa fedha, mali na rasilimali kwa ajili ya shughuli za kisiasa na kiutawala kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar unaofanywa na wadaiwa ni kinyume cha sheria na ni batili.
Vilevile wanaomba Mahakama isitishe kwa muda shughuli zote za kisiasa mpaka maagizo ya Mahakama yatakapotekelezwa, na zuio la kudumu dhidi ya matumizi ya mali, fedha na rasilimali za chama hadi walalamikiwa watakapotekeleza matakwa ya sheria husika na gharama za kesi.