Abood awajibu wakosoaji, aahidi maendeleo Morogoro Mjini

Morogoro. Mgombea ubunge  Morogoro Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdul-Aziz Abood, amewajibu wakosoaji wake wanaodai kuwa hajafanya kazi katika kipindi cha miaka 15 aliyokuwapo bungeni, akibainisha kuwa maendeleo yaliyopatikana jimboni humo ni ushahidi wa kazi zake.

Abood ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 29, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni za CCM katika Kata ya Kichangani, akisisitiza kuwa iwapo wananchi watampa ridhaa tena katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, atakamilisha maeneo yaliyosalia.

Amesema moja ya mafanikio makubwa ni upanuzi wa huduma za kijamii, hasa sekta ya nishati ya umeme, ambapo hadi sasa upatikanaji wake umefikia asilimia 85 katika jimbo hilo.

“Kwenye umeme bado yapo maeneo ya pembezoni hayajapata. Tumefikia asilimia 85 na tukirudi tena tutakamilisha asilimia 15 zilizobaki. Maeneo mengi ya pembezoni tayari nguzo zimeshaanza kusambazwa. Halafu unasema Abood hajafanya kazi, unataka afanye nini zaidi ya maendeleo hayo? Mimi sisikilizi maneno, nachapa kazi, watase­ma mchana, usiku watalala,” amesema Abood.

Mwenyekiti wa CCM WIlaya ya Morogoro, Fikirini Juma (kulia) akimnadi Mgombea ubunge Jimbo la Morogoro mjini Abdul – Aziz Abood, kwa Wananchi wa Kata ya Kichangani wakati wa mkutano wa uzinduzi wa kampeni Kata hiyo. Picha na Jackson John.



Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kichangani kupitia CCM, Abdallah Mgomba amesema licha ya kuwapo kwa changamoto mbalimbali hasa kwenye sekta ya elimu, tayari ameandaa ilani ya kata itakayomsaidia mbunge kuyashughulikia matatizo baada ya kuchaguliwa.

“Nimepita sehemu nyingi za Kata ya Kichangani na kukusanya changamoto nyingi ikiwemo za elimu. Tayari nimeandaa ilani ya kata inayoelezea changamoto zetu zote, ambayo nitamkabidhi Mbunge Abood ili aanze nazo akipata ridhaa Oktoba 29,” amesema Mgomba.

Naye Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Simon Mkami amesema, “msisitizo wangu ni kwamba bado tutakuwa na mikutano ya kampeni katika kila tawi. Ni vyema wananchi wakajitokeza kwa wingi kwa sababu nia na madhumuni ni kukipatia ushindi wa kishindo Chama cha Mapinduzi Oktoba 29, 2025,” amesema Mkami.