Serikali, wadau kuunganisha takwimu na teknolojia kuboresha huduma za afya

Dar es Salaam. Wizara ya Afya imesema kipaumbele chake katika miaka ijayo ni kujenga mifumo thabiti ya takwimu na teknolojia itakayohakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kuachwa nyuma. Miongoni mwa mifumo inayotumika sasa ni Afy eMS na Unified Community System kwa ajili ya kuboresha afya ya jamiii, na GoTHOMIS, ambao unarahisisha ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za wagonjwa katika hospitali na vituo vya afya. Kupitia mfumo huo, watoa huduma wanaweza kufuatilia mwenendo wa huduma, kuandaa takwimu kwa wakati halisi na kuripoti moja kwa moja Wizara ya Afya.

Kauli hiyo imetolewa leo Septemba 29, 2025 na Wizara ya Afya kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe wakati akizungumzia maandalizi ya Mkutano wa Kitaifa wa Afya (THS 2025) utakaofanyika Oktoba 1 hadi 3, 2025 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo, unaoratibiwa na Tanzania Health Summit (THS), unatarajiwa kukusanya zaidi ya wajum-be 2,500 kutoka ndani na nje ya nchi, ukiwa na kaulimbiu: “Kuunganisha matumizi ya takwimu na teknolojia ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC).”

Dk Magembe amesema takwimu sahihi na za wakati ndizo msingi wa kufanya maamuzi bora ya kiafya, ikiwemo kutambua mapema milipuko ya magonjwa, kupanga rasilimali ipasavyo na kufuatilia mwenen-do wa afya katika jamii. “Kupitia ushirikiano na mashirika ya kimataifa, tunalenga kujenga mifumo thab-iti ya takwimu na kutumia teknolojia ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila kuachwa nyuma,” amesema Dk Magembe.

Amesema mkutano huo unatarajiwa kushirikisha wadau mbalimbali wa kimataifa wakiwemo WHO, UNICEF, UNFPA, Benki ya Dunia, taasisi za kidini na sekta binafsi ya afya.

Aidha, washiriki watajadili namna ya kuongeza matumizi ya teknolojia za kidijitali, mifumo ya kielektro-niki ya taarifa za wagonjwa na uchambuzi wa takwimu za kiafya ili kubadilisha utoaji wa huduma, hu-susan maeneo ya vijijini na yenye changamoto za upatikanaji wa huduma za rufaa. Amesema Wizara ya Afya inawaalika wadau wote wa sekta hiyo kushiriki kikamilifu katika majadiliano ya THS 2025 ili kuchangia mawazo, uzoefu na suluhu za pamoja kwa ajili ya kuboresha afya ya Watanzania.